Wednesday 6 November 2013

HUU NDIO MUSWAADA MAFAO YA WASTAAFU MWAKA 2013

 SERIKALI imewasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Mfuko wa GEPF wa Mafao ya Wastaafu ya Mwaka 2013 . Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii imetaka uondolewe mkanganyiko wa kanuni ya kukokotoa pensheni na kiinua mgongo, kwa kuwa na vigezo vinavyofanana ili mifuko yote itoe mafao sawa.

Aidha, imeshauri Msimamizi na Mdhibiti wa Hifadhi za Jamii (SSRA) kutengeneza utaratibu maalumu katika mifuko yote ya 
Hifadhi za Jamii na kubuni mfumo mpya na rahisi wa kutumia simu za mkononi, kuwafikia Watanzania wengi kujiunga na mifuko hiyo.

Kamati kupitia kwa Mwenyekiti wake, Jenista Mhagama ilitoa ushauri huo baada ya muswada kuwasilishwa bungeni na Naibu Waziri wa Fedha, Saada Salum.

“Fomula ya kukokotoa pensheni na kiinua mgongo kama inavyopendekezwa katika Muswada inatumia kigezo cha kigawo cha 1/580 wakati mifuko mingine inatumia 1/540, kadhalika kigezo kingine ni wastani wa mishahara wakati kuna mifuko inatumia mshahara wa mwisho,” alisema Mhagama, ambaye ni Mbunge wa Peramiho (CCM).

Alisema eneo hilo linaleta mkanganyiko mkubwa na linatakiwa kufanyiwa kazi haraka kuainisha mafao hayo kwa mifuko yote.

“Ni maoni ya Kamati kuwa na umuhimu mkubwa sasa wa kuwa na vigezo vinavyolingana ili mifuko itoe mafao sawa bila kuathiri mifuko yote husika tofauti na ilivyo sasa,” alisema.

Pia Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni a imependekeza kuwepo kwa vigezo sawa vya ukokotoaji wa pensheni na kiinua mgongo na kupendekeza kuwa nguvu ya ziada inahitajika kuwafikia Watanzania asilimia 80 wenye shughuli binafsi.

“Unapozungumzia sekta isiyo rasmi, tunagusa takribani Watanzania asilimia 80 wenye shughuli za kujiingizia kipato kama wavuvi, wakulima wadogo wadogo, madereva wa daladala, waendesha pikipiki, fundi waashi, fundi vyerehani, wamachinga na Watanzania wengine wajasiriamali, hawa wote wanapaswa kuangaliwa,” alisema Cecilia Pareso, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema).

Akichangia muswada huo, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) na Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Selukamba (CCM) ambao kwa nyakati tofauti pia walitaka kuwepo na vigezo sawa kwa mifuko yote ya hifadhi ya jamii ili itoe mafao sawa.

Serukamba alisema suala la kuwepo kwa vivutio vya kushawishi wanachama wengi kujiunga na mfuko fulani vinaweza kubaki lakini upo umuhimu wa lazima kuweka vigezo sawa vya mafao. Aliipongeza Serikali kwa Muswada huo akisema ni muhimu kwa maendeleo ya Watanzania.

Awali, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya kwa niaba ya Waziri mwenye dhamana Dk William Mgimwa, akitoa maelezo ya Muswada huo alisema unakusudia kufuta Sheria iliyopo hivi sasa ya Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini sura ya 51 iliyotungwa mwaka 1942.

Alisema lengo la kutunga upya sheria hiyo ni kutekeleza matakwa ya Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya Mwaka 2008 pamoja na Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2012 iliyofanya marekebisho katika sheria za Mifuko yote ya hifadhi ya jamii nchini.

habari ifuatayo ya Gloria Tesha  kwa hisani ya HabariLeo  gazeti—

0 comments: