Hawa ni wahamiaji wa haramu waliokamatwa usiku wa kuamkia leo mkoani Iringa
Hapa wakipata chakula kwani walikuwa kwenye hali mbaya kwa kukosa chakula
Hili ni gari ambalo lilikuwa likiwasafirisha kutoka jijini Tanga
Kamanda wa
polisi mkoa wa Iringa ACP Ramadhani Mungi alizungumza na waandishi wa
habari kuhusiana na kukamatwa kwa wahamiaji hao.
Na Mwandishi Wetu, Iringa
JESHI la Polisi mkoani Iringa limewakamata wahamiaji haramu 46 kutoka Ethiopia wakiwa njiani kuelekea Afrika Kusini.
Akizungumza na wanahabari mjini humo,
Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, ACP Ramadhani Mungi, amesema tukio hilo
limetokea majira ya saa 9:50 alfajiri ya leo katika eneo la Sheli ya
zamani kwenye kitongoji cha Geza Ulole, Kijiji cha Ruaha Mbuyuni, Tarafa
ya Mahenge wilayani Kilolo.
Kamanda Mungi amesema askari polisi
wakiwa kwenye doria waliwakamata wahamiaji hao haramu 46 kutoka Ethiopia
wakiwa kwenye gari lenye namba za usajili T342AJU aina ya Canter
likiendeshwa na Mbega Ally (37), kabila Mbondei na mkazi wa Tanga wakiwa
wanaelekea Afrika Kusini. Dereva wa gari hilo amekamatwa.
"Tumefanikiwa kuwakamata wahamiaji
hawa haramu baada ya kupata taarifa za kiitelijensia, hii inaonyesha
namna gani tulivyojipanga kuhakikisha tunawadhibiti wahalifu wote
wakiwemo wahamiaji haramu," alisema Mungi.
Mungi alisema kwamba, wahamiaji hao waliwekwa katikati ya matenga (maboksi) ya kubebea nyanya ambayo yalikuwa tu.
Wahamiaji hao haramu walikuwa
wamepakiwa kwenye Canter hiyo inayomilikiwa na Bw. Zuberi Kitojo mkazi
wa Tanga, ambapo wahusika walidai kwamba walikuwa wamepakia nyanya.
Mmoja wa wahamiaji hao haramu, Shiraom
Tadeu (20), amesema kwamba wamekimbia vita Ethiopia na kwamba walikuwa
wanaelekea Malawi kwenye makambi ya wakimbizi.
"Tumetumia siku 21 porini tukikwepa
vyombo vya usalama. Tumepitia Kenya na hatimaye kuingia Tanzania, kule
hali ni mbaya sana," alisema Tadeu na kuongeza kwamba wameshindwa kuomba
hifadhi ya ukimbizi Kenya kwa sababu hali ya amani ni tete, lakini kwa
hapa Tanzania hakuna kambi hata moja ya wakimbizi," alisema.
Tadeu, ambaye anaongea Kiswahili
kidogo, alisema kaka yake pia yuko kwenye kambi hizo za wakimbizi nchini
Malawi na ndiye amekuwa akiwasiliana naye tangu wanatoka Ethiopia. chanzo mjengwa blog
0 comments:
Post a Comment