Saturday 15 March 2014

YANGA YAGIIZA KIFAA KIPYA KWA AJILI YA KUPIMA UFANISI WA WACHEZAJI UWANJANI

KIFAA_0f1b5.jpg


    YANGA imeagiza kifaa maalumu nchini Ujerumani cha kupima ufanisi wa wachezaji wake uwanjani ambacho hakijawahi kuonekana kwenye ardhi ya Tanzania.
    Kifaa hicho kidogo kinachopachikwa kwenye jezi ya mchezaji upande wa nyuma, hutumika kwenye timu kubwa za Ulaya kutokana na gharama zake na kwamba ni teknolojia ya kisasa zaidi ambayo inahitaji umakini na utaalam.
    Kocha wa Yanga, Hans Pluijm ameuagiza uongozi kuingiza nchini kifaa hicho kinachoitwa Vis Track GPS. Kazi kubwa ya kipimo hicho ni kupima takwimu za ufanisi wa mchezaji kuanzia mazoezini mpaka kwenye mechi ambazo zinaweza kusaidia benchi la ufundi kujua kiundani afya, utendaji na ufiti wa mchezaji husika.
    Kipimo hicho pia kinapima umbali, mbio fupi za kasi na hata ulaji wa mchezaji.
    Kwa mujibu wa wataalam ni kwamba kipimo hicho kinafichua kila kitu na hata kama mchezaji hayuko fiti kinamuumbua.
    Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu alisema kocha ameusisitizia uongozi kwamba anahitaji mashine hiyo maalumu ya kukusanya taarifa za wachezaji ili kupandisha kiwango cha Yanga na kumrahisishia kazi.
    "Tutamletea kocha mashine hizo, nilishakwenda Ujerumani mwezi mmoja uliopita kwa lengo la kufuatilia na tumeridhika nazo na sasa tunafanya mchakato wa mwisho kuzileta nchini ili aanze kutumia,"alisema Ben

    "Mashine hizi zitakuwa ni nafasi nyingine kwa kocha kujua kila mchezaji anafanya nini kuanzia nidhamu ya uwanjani, kuheshimu muda, mazoezi anafanya kwa uwezo gani, kwenye mechi nako anajitumaje kulingana na majukumu aliyopewa na kocha, mwisho wa mwezi taarifa hizo zinafanyiwa tathmini na kutoa majibu ya umuhimu wa kila mchezaji,"alisisitiza kiongozi huyo.
    Kiongozi huyo alisema baada ya ripoti za mashine hizo kocha na benchi lake la ufundi litakaa na kujua mchezaji gani wa kukaa naye na yupi wa kumuondoa.
    Kwa mujibu wa wataalamu ambao ni madaktari kifaa hicho hakijawahi kutumia Tanzania.
    Juma Sufian ambaye ni daktari wa Yanga alisema: "Kifaa hicho ni kigeni kwa hapa nchini, hakuna timu ambayo imewahi kutumia, kazi yake kubwa ni kupima uwezo wa mchezaji hasa viungo katika kukimbia uwanjani kulingana na majukumu, vifaa hivyo vipo vya aina mbalimbali vikitofautiana katika majukumu kidogo."
    Mwanandi Mwankemwa ambaye ni daktari mkongwe wa tiba kwa wanamichezo alisema: "Hizo ni mashine zinazotumika kupima uwezo wa wachezaji katika kukimbia, kawaida mchezaji yeyote tunategemea atakimbia kilomita 12 akiwa uwanjani, hilo utalipima kwa kutumia kifaa kama hicho, vipo vya aina nyingi lakini mfano mzuri ni kile ambacho kinatumiwa Ulaya kuweza kutoa taarifa ya mchezaji husika amekimbia umbali gani utaliona hilo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, kunakuwa na mashine maalum."
    CHANZO:MWANANCHI

    0 comments: