Wednesday 12 March 2014

YANGA SC YATUA ALFAJIRI DAR, HASIRA ZOTE LIGI KUU, JUMAMOSI NA MTIBWA SUGAR MOROGORO


KIKOSI cha Yanga SC kinaondoka usiku mjini Cairo kurejea Dar es Salaam baada ya kutolewa katika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri Jumapili kwa penalti 4-3 baada ya sare ya jumla ya 1-1.
Ahly ilishinda 1-0 juzi baada ya dakika 90 Uwanja wa Border Guard (Haras Hodoud) na kufanya sare ya jumla ya 1-1 kutokana na Yanga pia kushinda 1-0 katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam na katika mikwaju ya penalti wakashinda 4-3.
Kocha wa Yanga SC, Hans van der Pluijm akizungumza na mshambuliaji wake Said Bahanuzi kabla ya mikwaju ya penalti. Bahanuzi ni kati ya wachezaji watatu wa Yanga SC waliokosa penalti pamoja na Oscar Joshua na Mbuyu Twite. 
Yanga ilitua jana Cairo ikitokea Alexandria na kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa wapinzani wao, Al Ahly kabla ya kualikwa chakula cha jioni kwa Balozi wa Tanzania nchini hapa, Mohammed Hamza.
Yanga SC ambao ni mabingwa wa Bara wamekubali matokeo na wanarejea Tanzania kuelekeza nguvu zao katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ili watetee ubingwa wao, ambako wanatarajiwa kutua majira ya Saa 12:00 asubuhi. 
Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Mhoalnzi Hans Van der Pluijm alisema kwamba vigogo wa Misri Al Ahly wamepoteza makali yao na si timu tisho tena ile aliyokuwa anaijua yeye, licha ya kuitoa timu yake juzi kwa penalti mjini Alexandria.
“Ilivyo, Al Ahly hii si timu kali tena ambayo sote tulikuwa tunaijua na ikiwa wataendelea kucheza kama hivi katika hatua ijayo, nina uhakika watataabika,”. 
“Tulikuwa karibu kuwatoa nje ya mashindano, lakini penalti ni mchezo wa bahati, na ninajivunia kiwango chetu,”alisema Pluijm baada ya mechi juzi.
 
Baada ya kuitoa Yanga SC, timu hiyo yenye maskani yake mjini Cairo itakutana na Al Ahly Benghazi kuwania kuingia Hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Yanga SC ambayo katika Ligi Kuu ya Bara inakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Azam FC katika mbio za ubingwa, itamenyana na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro Jumamosi.
 
Yanga SC inashika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu kwa pointi zake 38 kutokana na mechi 17, nyuma ya Mbeya City yenye pointi 39, baada ya kucheza mechi 21, wakati Azam ipo kileleni kwa ponti zake 40 baada ya mechi 18 
Na Salum Esry, Cairo
BIN ZUBARRY BLOG

0 comments: