Thursday 13 March 2014

YANGA SC WAIPA SIKU TANO ILALA KUWAPA KIBALI CHA UJENZI WA KISASA,

  VINGINEVYO WANAKINUKISHA NCHI NZIMA


KLABU ya Yanga SC imeipa siku tano Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam kutoa idhini ya kujenga Uwanja wa kisasa katika eneo la Jangwani mjini hapa, vinginevyo wataandamana kushinikiza suala hilo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu hiyo makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga mjini hapa mchana wa leo, Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Mzee Ibrahim Akilimali amesema wamebaini wanawekewa vikwazo na baadhi ya madiwani wa Manispaa hiyo.
Mishipa ya shingo; Mzee Akilimali katikati akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jangwani

“Jana kulikuwa na kikao cha baraza la madiwani na Yanga tuliomba tuhudhurie kikao hicho kwa sababu moja ya ajenda ilikuwa ombi letu la kuongezwa eneo na kibali cha ujenzi wa Jangwani City. Cha kusshangaza tulikatazwa kuingia kwenye kikao hicho na kukalishwa nje ya ukumbi kwa saa 10,” amesema Akilimali ambaye kwa mara ya kwanza alikuwa ameagizwa na uongozi wa Yanga azungumze na waandishi baada ya kuzuiwa katika mkutano mkuu uliopita wa wanachama wa klabu hiyo.

“Tumebaini tunawekewa kauzibe katika kufanikisha suala hili zuri na baadhi ya viongozi waliochaguliwa na wananchi. Tunakipenda chama chetu cha CCM na Yanga ndiyo mwanzilishi wa chama hicho kwa sababu hata Mwenyekiti wa Kwanza wa TANU (Mwl. Julisu Nyerere) ndiye aliyekuwa mwanachama mwenye kadi nambari moja ya Yanga.
Barua ya kuomba kuandamana

“Kama wanaaumua kumwaga mboga, na sisi tutamwaga ugali 2014 na 2015 kwa sababu Yanga imekuwa ikisaidia sana CCM kufanya vizuri. Uwanja wetu utakuwa na faida kubwa kwa serikali ambayo itapata mapato. Tunashangaa kuwekewa kauzibe na viongozi wetu.

“Tunawapa siku tano watupe jibu vinginevyo tutaomba kibali Jeshi la Polisi wanachama wa Yanga tuandamane dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye alifika hapa mwaka jana na kuagiza suala letu lishughulikiwe, au dhidi ya Mkuu wa Nchi kwa sababu watendaji wake wanakiuka Ilani ya Chama Tawala,” amesema zaidi Akilimali ambaye alikuwa amefuatana na viuongozi wengine wa Mabaraza la Wazee na Vijana wa Yanga.
Na Renatus Mahima, Dar es Salaam

0 comments: