Sunday 16 March 2014

ANGALIA RASASI ZINAVYOTUMIKA KUUA RAIA TARIME MKOA WA MARA

 
tarime_c4aa8.jpg
Tarime. Katika Kijiji cha Gomsala, Tarime mkoani Mara yupo Matuma Marwa (22), ambaye hakuwahi kufikiria kwamba siku moja atakuwa mlemavu pamoja na kuwa kila binadamu aliye hai ni mlemavu mtarajiwa.
Marwa alipatwa na ulemavu wa mguu Oktoba 9, mwaka jana, baada ya kupigwa risasi na polisi kwenye paja.
"Tulikuwa tunaelekea shambani, tukasikia milio ya risasi ikielekezwa tuliko sisi, risasi moja ilinipata kwenye paja na tangu wakati ule hadi sasa mguu wangu hauko sawa," alisema Marwa na kuongeza:
"Kazi yangu ni mkulima, ila kwa sasa nashindwa kulima kwa kuwa mguu bado unauma."
Marwa ni miongoni mwa watu waliopatwa na madhila yatokanayo na vita ya rasilimali baina ya wananchi na wawekezaji.
Marwa anaishi katika kijiji kilicho kandokando ya mgodi wa dhahabu wa North Mara.
Mgodi wa North Mara unamilikiwa na Kampuni ya African Barrick Gold tangu 2006 ilipoununua kutoka kwa Kampuni ya Placer Dome Tanzania, iliyokuwa ikimilikiwa na Afrika Mashariki Gold Mines.
Taarifa rasmi kutoka katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo, zinaonyesha kuwa, mbali na waliojeruhiwa na kupata ulemavu wa kudumu, pia wapo waliopoteza maisha kutokana na kupigwa risasi na polisi wanaolinda usalama katika migodi hiyo.
Matukio hayo na mengine ya unyanyasaji, yanawafanya wakazi wa maeneo haya kuchukulia uwepo wa madini ya dhahabu kama kero kwao na siyo neema au baraka kama ilivyotarajiwa.
Watu 24 wanadaiwa kwamba wamekwisha uawa kwa kupigwa risasi katika matukio, akiwamo mkazi wa Kijiji cha Nyangoto, Ryoba Maseke ambaye alipigwa risasi Julai 12, 2012.
Shangazi wa Maseke, Suzana Mwita anasema, marehemu alikuwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Mugumu, Serengeti na alifika kijijini kusalimia ndugu zake na hapo ndipo mauti yalipomkuta.
Mwaka huohuo, polisi pia wanadaiwa kwamba walimuua kwa risasi mkazi wa kijiji cha Kewanja, Kibwaba Ghati (23) katika tukio la Novemba 6, wakati wananchi wanaodaiwa kuvamia mgodi, walipokurupushwa na askari wa jeshi hilo.
CHANZO MWANANCHI

0 comments: