Saturday, 2 November 2013

HOJA YA KUMNG'OA MAKINDA YAPIGWA KOMBORA

 


Spika wa Bunge Anna Makinda akiongoza shughuli za Bunge Bungeni, mapema wiki iliyopita baadhi ya wabunge walikuja na hoja ya kutaka kumng'oa Spika huyo bungeni. Picha na Maktaba 

Na Neville Meena, Mwananchi
 
 

Dodoma. 
Mchakato wa kumng’oa madarakani Spika wa Bunge, Anne Makinda ambao umeanzishwa na Mbunge wa Nzega, Dk Khamis Kigwangalla (CCM), huenda usifanikiwe kutokana na vikwazo kadhaa vikiwamo kupingwa na baadhi ya wabunge wenye ushawishi mkubwa katika Bunge.

 Wabunge wameanza kumpinga hadharani kuhusu suala hilo ambalo jana mjadala wake uliyateka makundi ya wabunge waliokuwa wakihudhuria vikao vya kamati mbalimbali wakati wakiwa kwenye mapumziko.

Katika viwanja vya Bunge jana, gazeti hili liliwashuhudia Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM) na swahiba wake kisiasa, Kangi Lugola ambaye ni Mbunge wa Mwibara (CCM) wakikataa kusaini karatasi waliyopelekewa kuunga mkono kung’olewa kwa Spika.Baadaye kwa nyakati tofauti walisema “hoja hiyo haina mashiko” na kwamba hawakutumwa na wapigakura wao kuwania posho bungeni.Wabunge hao walikuwa wakirejea moja ya hoja za Dk Kigwangalla kwamba Makinda amekiuka kanuni kwa kuidhinisha malipo ya Sh430,000 kama posho kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, tofauti na wajumbe wa kamati nyingine ambao malipo yao ni Sh180,000 kwa siku.

Wengine wanaompinga Kigwangalla ni Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM) na yule wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR - Mageuzi), ambao pia walisema hawaoni sababu za msingi za kumwondoa Makinda madarakani.Rage kwa upande wake alisema haoni sababu za msingi za kutaka kumwondoa madarakani Makinda, wakati Kafulila alisema hilo ni suala la WanaCCM, kwani hata Spika aking’olewa atakayeziba pengo hilo hawezi kutoka upinzani.“Kama akitoka Makinda ataingia mtu wa opposition (upinzani) yeyote basi ningeweza kusaini, lakini ninachojua ni kuwa kama wakifanikiwa kumtoa watakaa kwenye Party Caucus (kikao cha chama) na watateua mwingine kutoka miongoni mwao na mimi simwamini mbunge yeyote wa CCM,” alisema Kafulila.

Filikunjombe na LugolaKwa upande wake Filikunjombe alisema hoja ya Dk Kigwangalla imejengwa katika msingi hafifu na kwamba “haizingatii masilahi mapana ya nchi, bali masilahi binafsi kwa mtazamo finyu wenye lengo la kujitafutia umaarufu”.“Bunge ni taasisi kubwa ambayo haiwezi tu kuingia katika mtego wa kuenguana kwa sababu ya posho. Watu wa Ludewa watanishangaa leo hii wakisikia kwamba eti nimesaini kumwondoa Spika madarakani kwa sababu ya posho,” alisema Filikunjombe na kuongeza: 

“Kama hoja ingekuwa ni kumtoa Spika kwa sababu anaipendelea na kuitetea Serikali bungeni kana kwamba yeye ni waziri, basi hoja kama hiyo mimi ningeweza kuiunga mkono, lakini siyo suala la posho”.Kuhusu hoja kwamba Spika Makinda alikiuka kanuni kwa kumteua Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti badala ya kuchaguliwa kwa kura, Filikunjombe alisema wanaopaswa kulalamika kwanza ni wajumbe wa kamati hiyo na siyo mtu mwingine yeyote.


Na Neville Meena, Chanzo Mwananchi gazeti

0 comments: