Wednesday 15 May 2013

UN YAHADHARISHA AFRIKA KUA KITUO CHA UGAIDI

 
UN YAHADHARISHA AFRIKA KUWA KITOVU CHA UGAIDI
Na Mwandish wetu

Kama Matukio ya kigaidi yanayoendelea kutokea Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na katika Ukanda wa Sahel ya Magharibi hayatadhibitiwa ,basi kuna hatari kubwa kwa Afrika kuwa kitovu cha Ugaidi na Uhalifu wa Kimataifa.

Umoja wa Mataifa, umetoa tahadhari hiyo, siku ya jumatatu wiki hii, wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa chini ya Urais wa Togo lilipofanya majadiliano ya wazi kuhusu Usalama na Amani Afrika; changamoto za mapambano dhidi ya ugaidi katika mazingira ya kudumisha Amani na usalama.

Ni katika majadiliano hayo, ambayo pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon alizungumza, ilielezwa wazi kabisa, kwamba, kama hatua madhubuti, shirikishi na endelevu hazitachukuliwa na Afrika yenyewe na kwa ushirikiano na Jumuiya ya Kimataifa na Taasisi mbalimbali, basi Afrika itageuka kuwa kitovu cha mashambulizi makubwa ya kigaidi.
Makundi ya kigaidi ambayo yanaelezwa kujijengea himaya kuanzia Afrika Mashariki hadi Afrika Magharibi ni pamoja na Al-Shabaab,Al-Qaida, Boko Haram na Ansar Eddine.

Karibu wazungumzaji wote waliochangia majadiliano hayo, akiwamo Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, licha ya kukiri kwamba vitendo vya kigaidi ni tisho kwa mustakabali wa Afrika na watu wake, lakini pia walieleza kwamba hakuna sababu yoyote inayoweza kuhalalisha vitendo vya kigaidi.

"Hakuna sababu yoyote inayoweza kuhalilisha ugaidi" akasema Balozi Manongi na kuongeza " Ugaidi ni tishio kwa maadili ya ubinadamu na ni tishio kwa maendeleo na ustawi wa nchi na watu wake".

Balozi Manongi, alieleza kwamba Tanzania bado inakumbuka vema matukio pacha ya kulipuliwa kwa Balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya mwaka1998. Matukio ambayo Balozi wa Kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Susan Rice naye aliyakumbushia wakati akitoa mchango wake.


Aidha Balozi Manongi alieleza kwamba, Tanzania pia katika siku za hivi karibuni imeshuhudia tukio jingine la kigaidi lililotokea Mkoani Arusha.

Akaeleza kwamba ni kutoka na matukio hayo na hususani hili lililotokea hivi karibuni, Tanzania kupitia Kiongozi wake Mkuu, Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete, imedhamiria kwa nvugu zake zote kuukabili uovu huo.

Pia alieleza mikakati mbalimbali ikiwamo ya kupitishwa kwa sheria za sera zinazolenga kudhibiti vitendo vya ugaidi na fedha haramu.

Wazungumzaji kadhaa pia walitaka kuwapo kwa juhudi za kina za kudadisi na kushughulikia matatizo ambayo kwa njia moja ama nyingine yanachangia kuibuka kwa makundi ya kigaidi.
Baadhi ya matatizo hayo ni pamoja na sababu ukosefu wa ajira kwa vijana wengi, umaskini uliokithiri, kutokuwapo kwa utawala wa sheria, mbinyo wa demokrasia, machafuko ya mara kwa mara , na ulinzi hafifu katika mipaka baina ya nchi na nchi. 

0 comments: