Thursday 23 May 2013

HALI YA VURUGU ZA MTWERA JANA ZA POTEZA MAISHA YA WATU


Hali ya usalama ndani ya Mji wa Mtwara ni tete, watu watatu wanadaiwa kupoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa huku milio ya mabomu ya machozi na bunduki vikisikika kila kona.

Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamed Kodi amethibitisha kupokea mwili wa mtu mmoja ukiwa umetobolewa kwa kitu kinachoaminika kuwa ni risasi na majeruhi wengi.

Idadi kamili ya vifo hadi sasa haijathibitishwa kwani habari nyingine zinadai kuwa watu wanne wameuawa akiwemo polisi aliyekuwa anakwenda kazini. Mganga Mkuu wa Habari kutoka Mtaa wa Majengo zinadai kuwa vijana wamevamia ofisi ya CCM kata na ofisi ya serikali ya Kata hiyo na kuanza kuzibomoa, pia nyumba ya mwenyekiti wa
CCM Manispaa ya Mtwara-Mikindani Ali Chinkawene imerushwa mawe.

Ofisi ya CCM Mtwara Vijini iliyopo eneo la Sabsaba nayo imechomwa moto na watu wasiojulikana.

Katika mtaa wa Magomeni kundi la vijana linadaiwa kuwasha tairi la gari moto katikati ya barabara, Mikindani inadaiwa kuwa ofisi ndogo ya mbunge wa Mtwara Mjini, Asnein Murji na ofisi ya CCM wilaya ya Mtwara Vijijini iliyopo Mtaa wa Sabasaba zimechomwa moto.

Shule za Msingi Shangani, Majengo wanafunzi walirejeshwa nyumbani mara baada ya mabomu ya machozi kuanza kurindima hewani.

Tangu asubuhi kama ilivyokuwa Mei, 17 mwaka huu mji wa Mtwara ulikuwa kimya, huduma nyingi za kijamii zilifungwa, ukiwemo usafiri wa Pikipiki, Daladala, usafiri wa kwenda wilayani, Maduka, Soko kuu na kituo kikuu cha Mabasi.

Hali hiyo imejitokeza kufuatia kusambazwa kwa vipeperushi na watu wasiojulikana vikiwataka wafanyabishara mjini hapa kusitisha huduma za kijamii ili wasikilize Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini juu ya hatima ya madai yao ya kupinga mradi wa usafirishaji wa gesi kutoka Msimbati hadi jijini Dar es Salaam kwa njia ya bomba.

Hata hivyo wakazi wengi wamekosa fursa hiyo baada ya matangazo yanayorushwa na televisheni ya Taifa (TBC1) kutopatikana kwa dishi za kawaida isipokuwa DSTV tangu leo jioni, hata hivyo matangazo yalirejea leo muda mfupi baada ya Wizara ya Nishati na Madini kusoma bajeti yake.

Vipeperushi kama hivyo vilisambazwa mwanzoni mwa wiki iliyopita na kusababisha huduma za kijamii kusimama siku ya Ijumaa, Mei 17, 2013 vikidai kuwa siku hiyo bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ingesomwa Bungeni hata hivyo haikusomwa.

Baadaye taarifa zilisema kuwa bejeti ya wizara hiyo ingesomwa Mei, 22 mwaka huu leo) hali iliyotoa nafasi kwa wandaaji wa vipeprushi hiyo kusambaza ujumbe mwingine wa kutaka huduma zisimame kwa siku ya leo na kesho kwa njia ya simu za mkononi na.

Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Mtwara Mikindani, Chinkawene amethibitisha kubomolewa kwa ofisi ya chama chake, ofisi ya kata na nyumba yake kurushiwa mawe.

“Ni kweli ofisi ya CCM, Ofisi ya Serikali ya Kata zimebomolewa, nyumba yangu imerushiwa mawe” aliongea Chinkawene kwa sauti ya chini na kukata simu

Wakati Mtwara mjini hali ikiwa si shwari, Kijijicha Msimbati ambako gesi asilia inachimbwa hali ni shwari na wananchi wanaendelea na kazi zao kama kawaida

“Maduka na soko limefunguliwa, huku hali shwari kabisa, ingawa msimamo wetu upo palepale, hatutaki gesi iende Dar es Salaam kwa njia ya bomba” alisema Juma Ayoub mkazi wa Msimbati

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa alisema taarifa kamili atatoa baadaye na kwamba kwa sasa anaendelea na oparesheni.

---
UPDATE/TAARIFA MPYA:

  • Habari za hivi punde zinasema gari lililobeba wanajeshi kutoka wilaya ya Nachingwea mkoani lindi limepata ajali eneo la Nanganga wilaya ya Masasi mkoani Mtwara jioni hii, na wanajeshi 3 wamekufa huku 23 wakijeruhiwa. Habari za siri zinadai kuwa majeruhi wanakimbizwa katika hospitali za Ndanda na Nyangao kwa matibabu. Inadaiwa wanajeshi hao walikuwa wanakujakusaidia kutuliza ghasia zinazoendelea. 
  • Mbwa wa polisi kutoka songea mkoani Rvuma wamewasili mkoani Mtwara kuimarisha ulinzi. Habari za ndani ya jeshi la polisi mbwa hao watatumika kukamata watia vurugu. Iakumbukwa kuwa tangu saa tano asubuhi mji wa Mtwara ulitawaliwa na milio ya mambomu na bunduki hadi saa 12 jioni ilipotulia, kwa sasa milio hiyo inaiskika mara chache baada ya nusu saa.
  • Katika hatua nyingine Watu 45 wanashikiliwa na polisi kwa vurugu za kupinga gesi kwenda Dar es Salaam kwa njia ya bomba zilizotokea leo. Kamanda wa Polsisi wa mkoa wa Mtwara Linus Sinzumwa amesema hakuna aliyekufa wala kujeruhiwa katika matukio yanayoendelea mjini hapa.Amesema kwa kiasi kikubwa jeshi lake limefanikiwa kutuliza ghasia na kwamba katika maeneo machache wanaendelea na kudhibiti hali hiyo. Kauli hiyo ya kamanda Sinzumwa inapinga na ya Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamedi Kodi aliyethibitisha kupokea mwili wa mtu mmoja na wengine wengi kujeruhiwa.
 

0 comments: