Saturday 25 May 2013

AFISA HABARI WA BUNGE WA ZAMANI AFARIKI DUNIA AKIWA MASOMONI NJE YA NCHI

AFISA HABARI WA BUNGE WA ZAMANI AFARIKI DUNIA



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
BUNGE LA TANZANIA
TANZIA
MAREHEMU NDG. ERNEST ZULU
(1957 – 2013)
Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashililah, anasikitika kutangaza kifo cha mtumishi wa Bunge, ndg. Ernest Zulu, Afisa Habari Mkuu, aliyefariki dunia tarehe 23/05/2013 akiwa masomoni nchini Malaysia, kwa maradhi ya kichwa yaliyomsumbua kwa muda mrefu.
Mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu kuja Tanzania kwa mazishi inaendelea. Taarifa ya ratiba kamili ya maziko itatolewa pindi mipango hiyo itakapokamilika. Ndg. Ernest Zulu alizaliwa tarehe 10 Julai, 1957 Songea Ruvuma na alipata Elimu ya uandishi wa Habari katika chuo cha Uandishi wa Habari cha TSJ (siku hizi SJMC) Jijini Dar es salaam na baadae kuajiriwa na shirika la Utangazaji la Tanzania (RTD) mwaka 1976 kama mwandishi wa Habari Msaidizi na hatimae kupandishwa cheo na kuwa Mwandishi wa Habari kabla ya kuhamia shirika la magazeti ya Chama la Uhuru na Mzalendo kama  Mwandishi Mwandamizi mwaka 1985, ambapo mwaka 1986 hadi 1987 alipata fursa ya kusomea masomo ya Uandishi wa Habari za Kimataifa huko nchini Urusi.
Mwaka 1991 aliajiriwa kama Mhariri Msaidizi katika gazeti la The Express kabla ya kujiunga na Sauti ya Ujerumani ambako alifanya kazi kama Mwandishi Mwandamizi kuanzia mwaka 1995.
Mwaka 1998 aliajiriwa na Ofisi ya Bunge kwa Cheo cha Afisa Habari Mwandamizi ambapo mpaka mauti inamkuta alikuwa Afisa Habari Mkuu daraja la pili.
Ndg. zulu alikwenda masomoni nchini Malaysia Julai, 2010 katika chuo kikuu cha Taylor akichukua Shahada ya kwanza ya Mawasiliano na usimamizi wa vyombo vya habari ambapo alitarajiwa kumaliza masomo yake mwaka huu Julai.
Marehemu ameacha Mjane na watoto Wanne.
Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu mahala pema Peponi. Amina!
Imetolewa na Idara ya Habari,
Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa
Ofisi ya Bunge
DODOMA
24 Mei, 2013

0 comments: