Monday 13 May 2013

barafu za kuhifadhia maiti ni tatizo wilayani bunda.


WANANCHI wilayani Bunda mkoani Mara wamelalamikia kitendo cha Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda (Bunda-DDH) kukosa barafu kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.
Walisema hali hiyo imekuwa ikiwalazimu watu wanaofiwa ndugu zao kupeleka maiti katika hospitali za nje ya wilaya hiyo, zikiwemo Hospitali ya Rufaa Bugando, Shirati, Tarime na Hospitali ya Mkoa wa Mara iliyoko mjini Musoma.
Wakizungumza  kwa nyakati  tofauti jana, wananchi hao walisema hiyo ni kero kubwa na wamekuwa wakiingia gharama kubwa.
Walisema chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Bunda-DDH kwa kipindi kirefu hakina ubora kutokana na kutokuwa na jokofu la kufanya maiti zisiharibike.
“Hii hospitali imeshapoteza umaarufu wake iliyokuwa nao wakati inaanzishwa, chumba cha kuhifadhia maiti hakina ubora kabisa... hakuna friji, tunaangaika kutunza miili ya marehemu, sasa tunaipeleka nje ya wilaya kwa gharama kubwa,” alisema mwananchi mmoja wa mjini Bunda.
Aidha, walisema sio vema hospitali teule kukosa huduma hiyo na kwamba pia kituo cha afya Manyamanyama, ambacho sasa kimepandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Wilaya ya Bunda, pia hakina huduma hiyo.
Akizungumza kwa njia ya simu, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Bunda-DDH, Dk. Karekamo, alisema tatizo hilo ni la muda mrefu na kwamba linashughulikiwa.

0 comments: