Sunday 26 May 2013

PACHA WATANO WAFARIKI DUNIA RUVUMA

 PACHA WAFARIKI DUNIA


WATOTO pacha wote watano waliozaliwa juzi katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma wamefariki dunia.
Pacha hao walizaliwa salama juzi kwa kufanyiwa upasuaji kutoka kwa mama yao Sophia Mgaya (28), mkazi wa Ruhuwiko mjini hapa.
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Dk. Benedict Ngaiza, alisema kuwa watoto hao wameishi kwa saa kumi tu na kufariki dunia kutokana na kuzaliwa na uzito mdogo wa chini ya kilo moja.
Dk. Ngaiza alibainisha kuwa watoto wote wanaozaliwa wakiwa na uzito mdogo, nafasi yao ya kuishi ni ndogo sana.
Hata hivyo, hali ya mama wa watoto hao inaendelea vizuri ingawa bado amelazwa katika hospitali ya mkoa akiendelea kupata matibabu.
Tukio la kuzaliwa kwa pacha hao ambalo halijawahi kutokea katika hospitali hiyo lilitokea juzi majira ya saa 4 asubuhi, huku mtoto wa kwanza akiwa na uzito wa gramu 730, wa pili 810, wa tatu 670, wa nne 820 na wa tano 430.
Watoto watatu walikuwa wa kiume, wawili wa kike na huu ulikuwa mzao wa pili kwa mwanamke huyo.
Katika mzao wa kwanza wa mama huyo ambaye ni mwalimu, alijifungua mtoto mmoja.

0 comments: