Sunday 26 May 2013

SIASA YA TANZANIA (BONGO)PROFESA LIPUMBA AIBUA JIPYA NA ZITO

PROFESA LIPUMBA AIBUA JIPYA NA ZITO



http://www.ippmedia.com/media/picture/large/Lipumba(30)(2).jpgMWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ameibua suala zito akikihusisha chama chake na “kumnusuru” Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu uliopita.

Tanzania Daima limefahamishwa kuwa Profesa Lipumba alitoboa siri hiyo katika Msikiti wa Idrissa, Kariakoo, jijini Dar es Salaam, alikokwenda kuswali swala ya Ijumaa, miezi kadhaa iliyopita.

Kwa mujibu wa video ya tukio hilo, ambayo gazeti hili lina nakala yake, Profesa Lipumba alikaribishwa kuzungumza na waumini hao mara baada ya utangulizi uliotolewa na Imamu wa msikiti huo, Sheikh Ali Basaleh, aliyemtaka awaeleze Waislamu hali ya kisiasa nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Huku akisisitiza juu ya umuhimu wa mshikamano wa kiimani, Profesa Lipumba alianza kwa kuzungumzia matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2010, na ushindani mkali wa kisiasa uliokuwapo.

Alisema hawaoni matunda ya jitihada walizofanya kumnusuru Rais Kikwete asishindwe, kwani hata chini ya uongozi wake, Waislamu wameendelea kutothaminiwa.

“Ninyi masheikh mnajua vizuri zaidi hali ya kisiasa ilivyokuwa, kwamba ilibidi zifanyike juhudi za makusudi ili kuokoa jahazi. Lakini pamoja na kuliokoa jahazi, hali halisi inaonyesha mpaka sasa hakuna matunda yoyote yaliyopatikana, na tupo katika mtihani mgumu zaidi,” alisema.

Katika hali ambayo inasemekana ushindi wa Rais Kikwete ulipatikana kwa mbinu, huku wengine wakiituhumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa ilimnusuru mgombea wa CCM, kauli hii ya Profesa Lipumba inadokeza kwamba anajua mkakati zaidi wa kazi ya Tume ya Uchaguzi.

Katika hali isiyo ya kawaida, Profesa Lipumba anaonekana kuhamasisha Waislamu kujipanga akisema “wenzetu wameanza kujipanga” kuelekea 2015.
 
CHANZO: TANZANIA DAIMA JUMAPILI
 

0 comments: