Tuesday 28 May 2013

SELIKALI IANGALIE USALAMA WA WAANDISHI WA HABARI WAWAPO KAZINI


Kajubi MukajangaKATIBU Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Kajubi Mukajanga, ameiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuchukua hatua za ziada za kuwahakikishia waandishi wa habari usalama wawapo kazini.

Mukajanga alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumzia vurugu za masuala ya gesi zilizoibuka wiki iliyopita mkoani Mtwara.

Alisema MCT inasikitishwa na kilichojiri mkoani humo hasa wananchi kupoteza maisha, mali kuharibiwa vibaya na amani kutoweka huku maisha ya baadhi ya waandishi wa habari yakiwa hatarini.

Alisema baraza hilo lilizungumza na waandishi wa habari wa magazeti ya Serikali ya Dailynews na HabariLeo yanayomilikiwa na Kampuni ya Standard Newspapers (TSN) Ltd, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Uhuru na Mzalendo ambao katika vurugu hizo pamoja na kuharibiwa mali zao walilazimika kukimbilia mafichoni kuokoa maisha yao.

Aliwataka wananchi kutambua kwamba kazi ya uandishi wa habari ina misingi yake.

“Jamani si kila kitu kinaandikwa au ni habari sasa hawa walishambuliwa eti kwa sababu tu hawakufanya yale ambayo wananchi wanayataka hii si sahihi, mbona mkulima wa karanga akilima mahindi hashambuliwi kwa kufanya tofauti.”

Aliiomba Serikali iweke utaribu mzuri wa kuhakikishia waandishi wa habari wanakuwa salama wanapokuwa kazini huku akisisitizia wamiliki wa habari nao kuwa makini na matamshi wanayotoa ili kutoweka rehani maisha ya waandishi.

0 comments: