Tuesday 28 May 2013

MBUNGE WA CCM AMKACHA PINDA

Na Haika Kimaro na Mary Sanyiwa, Mwananchi  (email the author)

 
Waziri Mkuu alitembelea Ofisi ya CCM Mtwara Vijijini, Mahakama ya Mwanzo ya Mitengo, Ofisi ya Kata ya Mtonya Mikindani, Ofisi ndogo ya Mbunge (Murji), Baa ya Mukuzi, nyumba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa na ya Mbunge wa Mtwara Vijijini.Mtwara. Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnain Murji ameikacha ziara ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokuwa akitembelea maeneo yaliyoathiriwa na vurugu zilizotokea mkoani hapa wiki iliyopita.
Katika ziara yake, Waziri Mkuu alitembelea Ofisi ya CCM Mtwara Vijijini, Mahakama ya Mwanzo ya Mitengo, Ofisi ya Kata ya Mtonya Mikindani, Ofisi ndogo ya Mbunge (Murji), Baa ya Mukuzi, nyumba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa na Nyumba ya Mbunge wa Mtwara Vijijini, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia ambazo zilishambuliwa katika vurugu za mwanzo.
Akizungumzia sababu za kukacha ziara hiyo, Murji alisema: “Ni kweli nilialikwa lakini kilichonifanya nisiungane na Waziri Mkuu ni ratiba kutokuonyesha kutembelea maeneo ya wananchi waliopatwa na maafa.
“Ratiba ile ilionyesha Waziri Mkuu atatembelea maeneo ya viongozi na Mahakama pekee bila kutembelea maeneo ya wananchi ndiyo sababu iliyonifanya nisihudhurie, wananchi wasingenielewa. Wangenigeuka na wangeniona nimewasaliti.
“Kwa kuwa nipo upande wa wananchi, nisingeweza kutembelea maeneo ya viongozi wa Serikali pekee lakini kesho (leo) wakati Waziri Mkuu akitembelea walioathirika na mimi nikiwa Mbunge wa Mtwara Mjini nitatembelea maeneo yote ya wananchi wangu waliokumbwa zahama hiyo.”
Murji alisema sababu ya kukataa gesi isitoke ni kutokana na nafasi nyingi za ajira kupatiwa wananchi wa nje kwa asilimia 90 huku asilimia 10 pekee ikibaki kwa wananchi wa Mtwara hali inayowafanya wananchi wasijue ni nini kitakachofuata baada ya gesi kupelekwa Dar es Salaam.
“Ni kweli wawekezaji ni wengi wanataka kuwekeza Mtwara na kama tulivyoelezwa kuna maombi ya wawekezaji 45, viwanda vingi vitakuja lakini ukiangalia upande wa ajira asilimia 90 zote zimeenda kwa watu wa nje,” alisema Murji.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Joseph Simbakalia, wakuu wa wilaya za mkoa huo, Kamishna wa Polisi (Operesheni), Paul Chagonja, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara, Mohamed Sinani na baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Akitoa maelezo ya tathmini ya mali zilizoungua Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mtonya, Yusuph Kaliwanje alimweleza Waziri Mkuu kuwa uchomaji wa majengo hayo ulianza saa nane mchana. Alisema ofisi ya kata hiyo yenye thamani ya Sh32 milioni, ilichomwa moto pamoja na nyaraka mbalimbali na samani.
Pia alisema vibanda mbalimbali vya wafanyabiashara pamoja na mali zilizoharibiwa zina thamani ya Sh33 milioni. Alisema tathmini ya hasara ya Ofisi ya Mbunge bado haijajulikana.


Na Haika Kimaro na Mary Sanyiwa, Mwananchi gazeti  
 

0 comments: