Friday 31 May 2013

JAPAN YA TANGAZA KUSAIDIA TANZANIA MABILIONI

Picture
Rais Jakaya Kikwete akiambatana na mke wake Mama Salma tarehe 30. 5.2013 wakitembelea makumbusho ya karakana ya sayansi ya TOSHIBA iliyoko huko Kawasaki karibu na Tokyo nchini Japan inayohusika na utengenezaji wa injini za treni na vifaa vingine vye elektroniki wakiangalia laptop ya kwanza pamoja na calculator iliyotengenezwa na kampuni hiyo mwaka 1985. Rais Kikwete yupo nchini Japan kuhudhuria mkutano wa tano wa uhusiano wa kiuchumi kati ya Japan na Africa.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Japan imetangaza misaada na mikopo ya mabilioni ya fedha kusaidia uchumi na maendeleo ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kugharamia uboreshaji wa miundombinu, ujenzi wa miradi ya barabara, ujenzi wa miradi ya maji, uanzishwaji wa skimu ndogo ndogo za umwagiliaji na uboreshaji wa kilimo cha mpunga.

Waziri Mkuu wa Japan, Mheshimiwa Shinzo Abe ametangaza hatua hizo za kuunga mkono jitihada za maendeleo za Tanzania wakati alipokutana na kufanya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Viongozi hao wawili wamekutana ofisini kwa Mheshimiwa Abe leo, Alhamisi, Mei 30, 2013, mjini Tokyo kwenye 
siku ya pili ya ziara ya wiki moja ya Rais Kikwete katika Japan ambako miongoni mwa mambo mengine amealikwa kuhudhuria Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Kujadili Maendeleo ya Afrika wa Tokyo International Conference on African Development (TICAD – V) unaoanza Yokohama, mji wa pili kwa ukubwa katika Japan, keshokutwa, Jumamosi, Juni Mosi hadi 3, 2013 na kuhudhuriwa na viongozi wa nchi za Afrika na washirika wa maendeleo wa Bara hilo.

Miongoni mwa miradi ambayo Japan imekubali kugharimia ambayo baadhi yake inaendelea kujengwa ama karibu inaanza kutekelezwa ni pamoja na Mradi wa Maji wa Mkoa wa Tabora, Mradi wa Kuboresha Usafiri katika Mkoa wa Dar Es Salaam ambao ni pamoja na kupanuliwa kwa Barabara ya Gerezani na Ujenzi wa Daraja Jipya kwenye barabara hiyo, Mradi wa Kuendeleza Kilimo cha Mpunga nchini na Mradi wa Awamu ya Pili ya Kuongeza Uwezo wa Serikali za Mitaa kwa Njia ya Mafunzo.

Miradi mipya ambayo Japan itagharimia ni pamoja na Mradi wa Kuendeleza Miundombinu, Mradi wa kujenga skimu ndogo za umwagiliaji, mradi wa ujenzi wa barabara ikiwa ni pamoja na kugarimia ujenzi wa barabara
katika milango ya kimataifa ya Mwara, Dodoma na Iringa na Mpango wa 10 wa Kuunga Jitihada za Kupunguza Umasikini.

Wakati wa mazumgumzo hayo, Waziri Mkuu Abe pia ametangaza kuwa Japan itagharamia ujenzi wa barabara za juu kwa juu (fly-overs) kwenye makutano ya barabara za TAZARA na Ubungo, ujenzi wa mtambo wa
kuchakata umeme wa Kinyerezi ambako unatekelezwa kwa mpango wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPF).

Waziri Mkuu Abe pia ameitaka Tanzania na Japan kukamilisha “haraka iwezekanavyo” majadiliano ya kufikiwa kwa makubaliano ya kulinda uwekezaji kati ya nchi hizo mbili ili kufungua njia za uwekezaji zaidi
katika uchumi wa Tanzania kutoka Japan, moja ya mataifa tajiri zaidi duniani.

Mheshimiwa Abe ameiomba Tanzania kuunga mkono jitihada za nchi hiyo kujiunga na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) chini ya mageuzi makubwa yanayotarajiwa kufanyika kwenye mfumo wa Umoja huo.

Rais Kikwete alijibu ombi hilo la Mheshimiwa Abe kwa kusema:
“Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaunga mkono moja kwa moja jitihada za Japan kujiunga na Baraza la Usalama kama mwanachama mwenye kura ya turufu. Unajua msimamo wetu kuhusu jambo hili siku nyingi.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU
DAR ES SALAAM
30 Mei, 2013
 

0 comments: