MSHAMBULIAJI wa Ujerumani, Thomas Muller amesema
kamwe hajawahi kufungwa na timu ambayo ndani yake yupo Lionel Messi na atapenda
kuendeleza hilo wakati watakapokutana na Argentina katika mechi ya fainali ya
kombe la dunia siku ya jumapili.
Muller amefurahia michuano ya mwaka huu ya kombe
la dunia kwa kufunga magoli matano
katika mechi tano alizocheza mpaka sasa na magoli kama hayo yalimfanya
abebe kiatu cha dhahabu nchini Afrika kusini mwaka 2010.
Nyota huyo wa Bayern Munich alisema yeye na
wachezaji wenzake watafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanatwaa kombe la
dunia kwa mara ya kwanza ikiwa imepita miaka 24.
“Itakuwa muhimu sana kucheza kwa juhudi kubwa,
hususani kujilinda. Unatakiwa kuwa makini kumlinda Lionel Messi”.
“Tumecheza dhidi ya Messi mara kadhaa. Sijawahi kufungwa mchezo wa
mashindano na yeye”.
“Hatujawahi kwenda Rio de Janeiro, bado kwangu
mimi sababu pekee ya kwenda pale ni kushinda kombe la dunia”.
Ujerumani iliifunga Brazil mabao 7-1 katika mechi
ya nusu fainali, lakini Muller anaamini mechi ya jumapili Maracana itakuwa
ngumu na kipimo kizuri kwa kikosi cha Joachim Loew.
“Sijui mechi itakuwaje siku ya jumapili, lakini
sitarajii kama itakuwa 5-0 kwa kipindi cha kwanza,” alisema.
“Inaweza kuwa nzuri, labda itakuwa ngumu kama
ilivyokuwa dhidi ya Algeria au Ufaransa”.
“Tutafanya kila linalowezekana ili kushinda kombe
la dunia”.
0 comments:
Post a Comment