AZAM FC inatarajia kucheza mechi ya kujipima uwezo
kesho asubuhi dhidi ya maafande wa jeshi la kujenga taifa kutoka mkoani Pwania,
Ruvu Shooting katika uwanja wa Azam Complex.
Afisa habari wa klabu hiyo, Jafar Idd Maganga
amesema kikosi cha Azam kinaendelea vizuri na mazoezi chini ya kocha mkuu, Mcameroon,
Joseph Marius Omog ambapo kila wiki wanahitaji kucheza mechi ya kirafiki.
“Tunaendelea vizuri na mazoezi. Ushindani umekuwa
mkubwa kwa wachezaji. Unajua kipindi hiki ni kigumu kwa wachezaji, kila mtu
anahitaji kufanya vizuri ili kupata namba”. Alisema Jafar.
“Tumekuwa tukicheza mechi za kirafiki kwa lengo la
kujua kama wachezaji wanaelewa yale yanayofundishwa”.
“ Kwahiyo kesho tutakuwa na mechi ya kirafiki
dhidi ya Ruvu Shooting, moja ya timu nzuri, yenye vijana wenye uwezo mkubwa.
Wao watasafiri kuja kwetu”. Aliongeza Jafar.
Kikosi cha Ruvu Shooting msimu uliopita
“Tumesajili wachezaji wengine, wote wanaonesha
kiwango kizuri. Hivyo inaonesha kutakuwa na ushindani mkubwa kikosini”.
Aidha, Jafar aliongeza kuwa kocha mkuu Omog
ameamua kuahirisha mpango wa kwendea nje ya nchi kuweka kambi, badala yake kwa
muda uliobaki wataendelea kufanya mazoezi Chamazi na kucheza mechi za kirafiki.
Kwa upande wao, Ruvu Shooting walisema maandalizi
kwa ajili ya mechi hiyo yamekamilika na kesho watawaonesha mabingwa hao wa ligi
kuu namna ya kucheza soka.
Afisa habari wa klabu hiyo, Masau Bwire alisema kikosi chao kipo vizuri baada ya kusajili wachezaji kadhaa, hivyo kesho watawaonesha Azam kuwa wao ni watu makini.
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0 comments:
Post a Comment