Jeshi la Polisi Mkoani hapa limeendelea kupambana na wahalifu wa
madawa ya kulevya ambapo juzi limefanikiwa kukamata magunia 20 ya
madawa hayo aina ya bangi.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas alisema
kwamba, madawa hayo yalikamatwa tarehe 23.07.2014 muda wa saa 2:30 usiku
wilayani Longido katika kijiji kiitwacho Olteres.
Kamanda Sabas alisema kwamba, mafanikio hayo yalipatikana baada
ya Jeshi hilo kupata taarifa toka kwa raia wema zikieleza kwamba kuna
watu wanayasafirisha kwa kutumia wanyama aina ya Punda.
Mara baada ya taarifa hiyo ndipo askari wa Jeshi la Polisi kwa
kushirikiana na askari wa kampuni ya Jumuiya ya Jamii inayojishughulisha
na Ulinzi wa wanyamapori na mazingira kambi ya Enduimet walianza
kuwafuatilia kuanzia saa 8:00 Mchana na kufanikiwa kuona nyayo za punda
pamoja na binadamu ambazo zilikuwa zinaonyesha zimetokea Oldonyasambu
kuelekea Namanga.
Kamanda Sabas aliongeza kwa kusema kwamba uchunguzi wa Jeshi la
Polisi ulibaini kwamba magunia hayo yanayokadiriwa kuwa na kilogramu 80
kila mojawapo yalikuwa yanapelekwa nchi jirani ya Kenya yalipatikana
baada ya msako uliofanywa na askari hao kwa takriba saa 4 na dakika 30
ambapo yalikuwa yametelekezwa kijijini hapo huku wahusika wakitoweka
kusikojulikana.
Hata hivyo Jeshi hilo Mkoani hapa linaendelea na upelelezi juu
ya tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwasaka watuhumiwa wa tukio hilo huku
doria ikiendelea ili kuweza kudhibiti wahalifu wote wanaodhubutu kupita
njia za panya baada ya kuona wanabanwa katika barabara kuu.
Jeshi la Polisi mkoani hapa linaendelea kutoa shukrani kwa
wananchi wanaotoa taarifa za mara kwa mara juu ya uhalifu na wahalifu na
kuomba waendelee kujitokeza ili taarifa hizo zifanyiwe kazi na hatimaye
kufanikisha kupunguza uhalifu wa maeneo mbalimbali ya Mkoa huu.
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
0 comments:
Post a Comment