WAJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba
walioshiriki katika mkutano wa majadiliano uliondaliwa na Mtandao wa
Wanawake na Katiba wameahidi kupaza sauti kupigania masuala ya haki za
wanawake na usawa wa kijinsia pamoja na kusimamia usawa kwa jamii yote
juu ya mgawanyo wa rasilimali ardhi, elimu, uongozi na huduma za
kijamii.
Kauli hiyo imetolewa leo na baadhi
ya wajumbe hao walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari, katika
Hoteli ya Golden Tulip ya jijini Dar es Salaam eneo unapofanyika mkutano
huo uliomalizika leo jioni. Mjumbe wa Bunge Maalum, Valerie Msoka
alisema majadiliano walioshiriki yamewawezesha wajumbe kurudi katika
majadiliano ya awamu ya pili wakiwa na nguvu mpya huku wakiyapa
kipaumbele na kuhakikisha kuna usawa katika masuala ya ardhi, elimu,
rasilimali, uongozi na huduma za kijamii.
Alisema kwa muda wa mwanzo ambao
wajumbe walipata kuhudhuria na kujadili baadhi ya ibara wamepata uzoefu
kidogo jambo ambalo kwa kipindi cha pili litawasaidia kuongeza ujasiri
wa kuendeleza hoja zao za msingi zikiwemo walizoshiriki kuzijadili
katika mkutano huo. Kwa upande wake Mjumbe wa Bunge Maalum, Fedrick
Msigala alisema mkutano huo umewawezesha wajumbe kujenga zaidi uelewa
juu ya masuala ya usawa wa jinsia na kuangalia namna wajumbe wanaweza
kuyatetea kuingizwa kwenye mchakato wa uundaji katiba mpya unaoendelea.
“…Mimi kama mwakilishi wa walemavu
natambua namna ambayo wanawake walemavu wanavyo athirika na vitendo vya
ukatili na manyanyaso yote ambayo wanakumbana nayo…sasa semina kama hii
inatupa taarifa na uwezo pia wa kujenga hoja katika kutetea usawa wa
kijinsia kuingizwa vizuri kwenye ibara mbalimbali husika kwenye Katiba
Mpya,” alisema Msigala.
Naye mjumbe wa Mtandao wa Wanawake
na Katiba, Usu Mallya alisema majadiliano hayo kati ya Wabunge wa Bunge
Maalum la Katiba na Wajumbe wa Mtandao wa Wanawake na Katiba ni nafasi
muhimu kwani inawakumbusha wajumbe kupaza sauti juu ya haki za wanawake
na usawa wa kijinsia kuingizwa kwenye sheria mama ya nchi ambayo ni
katiba.
Alisema masuala ya haki za
wanawake na usawa wa kijinsia yakiingizwa katika jamii yataziwezesha
mamlaka husika kuwajibika na taasisi husika kusimamia kwa uhakika na
kuziwajibisha pale masuala hayo yanaposhindwa kutekelezwa kwa mujibu wa
maelekezo.
“…Muhimu pia ni kutambua umuhimu wa kusimika suala la usawa wa
kijinsia kwenye katiba ni kutokana na ukweli kwamba wanawake wanahusika
katika kulikamilisha taifa la Tanzania na wanamchango mkubwa licha ya
mfumo kuendelea kuwabana katika fursa mbalimbali,” alisema Bi. Mallya.
Alisema sasa umefika wakati fikra
potofu zitokomezwe ambazo zimekuwa zikiendelea kuwabana wanawake kwamba
hawawezi na kuambulia nafasi ndogondogo maeneo anuai ya vyombo vya
maamuzi ngazi zote.
“Nafasi kama hii ya kuwezesha
Wajumbe wa Bunge la Katiba waweze kuendelea kuyabeba haya masuala katika
mjadala utakaoendelea ni muhimu…na kwetu sisi tunachotegemea ni kwamba
haya masuala yataendelea kuwa ni sehemu ya msingi katika majadiliano
yanayoendelea kule bungeni, tunawaomba waandishi wa habari waendelee
kuzipa nafasi hizi hoja na tunawapongeza pia kwa kutuunga mkono,”
alisema Bi. Mallya.
Mkutano huo umetoka na maadhimio
ambayo wajumbe wataendelea kuyafanyia kazi, ikiwemo washiriki kuendelea
kuwasiliana na kupanua wingo wa kupaza sauti juu ya hoja walizozijadili
na kuyashirikisha makundi mengine katika kupaza sauti ili hoja
zilizojadiliwa zipate nafasi ya kuingizwa kwenye mchakato.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
0 comments:
Post a Comment