Wednesday, 23 July 2014

TFF HII TABIA YA KUONGEZA MUDA WA USAJILI NA KUPIGA KALENDA LIGI KUU ITAISHA LINI?


Rais wa TFF, Jamal Emil Malinzi aliaminiwa na Watanzania wengi kuongoza soka, lakini kuna changamoto nyingi zinazomkabili kiutendaji



SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) jana limetangaza kuongeza muda wa usajili kwa wiki mbili ili kuzipa klabu nafasi ya kukamilisha taratibu zinazotakiwa.
Katika taarifa yake, TFF ilisema hatua ya kwanza ya usajili inakamilika Agosti 17 mwaka huu badala ya Agosti 3 ya awali.
Kutokana na marekebisho hayo, kipindi cha uhamisho kinakamilika Agosti 17 mwaka huu wakati pingamizi itakuwa kati ya Agosti 19 hadi 26 mwaka huu.
Pia Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji itathibitisha usajili kati ya Septemba 1 na 2 mwaka huu. 
Uhamisho wa kimataifa, usajili wa wachezaji huru, na utatuzi wa dosari za usajili unatakiwa uwe umekamilika kufikia Septemba 7 mwaka huu. Uthibitisho wa hatua ya mwisho ya usajili utafanywa Septemba 15 mwaka huu.
Kwa upande wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2014/2015 itaanza Septemba 20 mwaka huu, na ratiba itatolewa mwezi mmoja kabla ya kuanza ligi hiyo.
Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa Simba sc, Zacharia Hans Poppe ameongezewe wiki mbili na TFF kukamilisha taratibu zinazotakiwa.

Utaratibu huu wa kuongeza-ongeza muda umezoeleka nchini Tanzania na kufikia hatua kuonekana kama ni ‘kasheria’ fulani. Mazoea hujenga tabia, ‘walishasemaga’ wazee wa zamani. Moja ya kanuni ya maisha ni kuzingatia muda na kufuata mipaka uliyojiwekea.
Kama umepanga kufanya kazi kwa saa nne, basi ikifika muda huo inabidi uache, labda kama kumetokea sababu ya msingi, hapo unaweza kuongeza muda zaidi.
Barani ulaya, sheria zinaheshimika sana ikiwemo hii ya dirisha la usajili. Siku zote sipendi kuifananisha Tanzania na Ulaya, hatuwezi kuwa kama wao, lakini kuna vitu vyepesi vya kuwaiga kama hili la kwenda na muda.
TFF wanaongeza muda wa usajili na ukisoma sababu yao ni kuzipa klabu nafasi ya kukamilisha taratibu zinazotakiwa. Kwani klabu haziwezi kukamilisha taratibu hizo ndani ya muda uliopangwa? lazima ziongezewe muda?
Haya sasa Seif Ahmed `Magari` (mwenyekiti wa kamati ya mashindano na mjumbe wa kamati ya usajili Yanga sc)  fanyeni yenu, TFF wamewapa muda wa wiki mbili zaidi wa kusaka wachezaji 

Kwa mtazamo wa haraka haraka, kuongeza muda imekuwa mazoea. Sidhani kama ni sheria, lakini TFF wanaongozwa zaidi na busara kufanya maamuzi na sio sheria.
Unaweka siku ya mwisho ya usajili (Deadline) kuwa ni Julai 15, muda unafika unatokea hadharani ukisema: “Nimeongeza muda kwa wiki mbili ili klabu zikamilishe taratibu”.  Kwanini wasikamilishe ndani ya muda uliopangwa na kama watashindwa kwanini wasichukuliwe hatua au waachwe na timu zao `mbofu mbofu`.
Ni jambo rahisi tu kubaki katika misingi ya kanuni ili tuepukane na mazoea. Naamini wapo viongozi wa klabu huwa hawahangaikii usajili ndani ya muda uliopangwa kwasababu wana uhakika kuwa TFF itaongeza muda.
Kiongozi hasajili, akiulizwa  kwanini? Utasikia muda bado upo, tunafanya mambo yetu polepole. Ukiangalia muda unaosema upo, unagundua unakaribia kwenye siku ya mwisho (Deadline). Ni rahisi kujua kuwa kuna baadhi ya watu wanakuwa wanajua kabisa kwamba TFF wataongeza muda.
Huku ni kuwazoesha watu kutofuata kanuni na sheria. Kwanini watu wazembee kwa madai ya kuongezewa muda.


Mabingwa Azam fc nao hawajakamilisha usajili?

Wenzetu hawana taratibu za hivyo. Siku ya mwisho ya usajili, makocha wanahaha kama hawajakamilisha. Unakumbuka usajili wa Mesut Ozil kujiunga na Asernal kitokea Real Madrid?. Aserne Wenger alijua kabisa  inakula kwake, muda umekwisha na hajafanya mambo.
Unadhani Wenger aliwahi kuwaza kuwa muda wa usajili utaongezwa?, lakini kwa Bongo ndio kwanza watu wanalala na kuendelea na maisha mengine, huku `Deadline` ikikaribia.
Ifike wakati TFF ibaki katika misingi ya kanuni ili kuondoa usemi wa `Hii ni Afrika` yaani `This is Africa`. Tusipende kujipa mazoea nje ya kanuni.
Kila siku tunajadili kuendeleza soka, tunaangalia upande mmoja wa tu yaani mpira wa uwanjani, hata suala la kuzingatia kanuni na sheria ni sehemu ya mchezo.
Leo hii huwezi ukawa unaongeza muda bila sababu ya msingi, mara ratiba inawekewa viraka, mara inasogezwa mbele zaidi bila kuwa na sababu ya msingi.
Kwa mfano mwaka huu ratiba imesogezwa kutoka Agosti 24 mpaka septemba 20 mwaka huu. Sababu kubwa ni kuipisha Yanga itakayoenda kushiriki kombe la Kagame nchini Rwanda kuanzia Agosti 8 mwaka huu.
Kama Yanga watafika fainali, maana yake watamaliza mashindano hayo Agosti 24 ambayo ndio siku ya fainali kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CECAFA siku ya jana.
Lakini kama Yanga watatolewa hatua ya makundi, maana yake watarudi nchini kati ya Agosti 17 au 18 kwasababu mechi ya mwisho ya makundi itakuwa Agosti 16 dhidi ya Coffee ya Ethipopia.
Kama watapambana na kufika fainali, maana yake Kagame ingemalizika siku ambayo ligi inaanza kwa mujibu wa kalenda ya awali ya TFF.
Lakini kwasababau hiyo ya kombe la Kagame, TFF wakasogeza ligi mpaka septemba 20. Ukiangalia hapa, ni siku 26 zaidi baada ya kagame kumalizika. Hivi sababu ni Kagame au ndo mpaka haya mambo ya usajili?
Wakati taarifa ya kusogeza mbele ligi kuu inatolewa na TFF, ilielezwa kuna sababu mbalimbali za kufikia maamuzi hayo, lakini kubwa ni kuisubiri Yanga.
Sababu mbalimbali hazikuweka wazi kwa kumbukumbu zangu, lakini sasa nimegundua kuwa ni pamoja na klabu kutokamilisha usajili.
Hii ni tabia isiyofaa kuendelea. Rais wa TFF, Bwana Jamal Emil Malinzi, umeaminiwa na Watanzania wengi, japokuwa kumekuwepo na dosari za hapa na pale kiutendaji, futa mazoea ya kutoka kwenye kanuni.
Sioni sababu ya kuongeza muda wa usajili, lazima tufuate kanuni. Najua ligi yetu ni fupi sana na ndio maana inapigwa pigwa kalenda, lakini kuna njia nyingine ya kufanya ikiwa ni pamoja na kurudisha mashindano kama Taifa Cup na mengineyo.
Nadhani kuna watu wa klabu wapo TFF, kwahiyo wanafanya maamuzi kwa maslahi binafsi na kuja hadharani kama TFF.
Watu hawa wanakuja na suala la kuongeza muda eti klabu hazijakamilisha taratibu. Mbona kuna timu zimemaliza kusajili?
Mazoea yana taabu. Ukishazoea kufanya kitu kinyume na taratibu, utaona kanuni na sheria ni adau yako.

                                      Ramadhani Karim!
 
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam

 

0 comments: