YANGA SC wataanza kampeni ya kusaka taji la kombe
la Kagame Agosti 8 mwaka huu dhidi ya wenyeji Rayon Sport katika dimba la
Amahoro mjini Kigali.
Hii itakuwa mechi ya kwanza ya mashindano kwa
kocha mkuu wa Wanajangwani, Mbrazil Marcio Maximo aliyetua Yanga mwaka huu
baada ya Mholanzi Hans van Pluijm kumaliza mkataba wake na kutimkia Saudi
Arabia sambamba na aliyekuwa msaidizi wake Charles Boniface Mkwasa `Master`
Hata hivyo kumetokea utata wa Yanga kushiriki
michuano hiyo kwa madai kuwa hawajapata barua rasmi ya mwaliko kutoka baraza la
vyama vya soka kwa ukanda wa Afrika mashariki na kati, CECAFA.
Afisa habari wa klabu ya Yanga, Baraka Kizuguto amekaririwa
jioni ya leo akisema wanasikia kwenye vyombo vya habari kuwa ratiba ya
mashindano imetoka na wamekuwa wakiendelea na maandalizi, lakini hajapata
taarifa rasmi kutoka kwa waandaaji.
“Sisi tumesikia mashindano yanafanyika na
tumeshaanza maaandalizi, lakini mashindano yanaanza lini, sisi hatujapata barua
rasmi na tunasikia kwenye vyombo vya habari,”. Alisema Kizuguto.
“Sisi hatuna taarifa, aidha mwaliko au ratiba.
Yawezekana taarifa inakuja, itakapofika sisi tutaongea”.
Wakati huo huo, Afisa habari wa CECAFA, Rodgers
Mulindwa amekaririwa akiwashutumu Yanga kuwa wanaogopa mashindano ya Kagame
kwasababu barua ya mwaliko walishatuma shirikisho la soka Tanzania, TFF.
“Yanga wanaogopa michuano, hawataki kucheza. Barua
tumeshatuma TFF. Mwaka jana walikataa kwenda Darful. Waende TFF, kama hakuna
mwaliko tutatuma tena”. Alisema Mulindwa.
Nao TFF wanasema mwaliko huo upo na CECAFA
walishatuma barua.
Katibu mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa amesema
taarifa zote wanashirikiana na Yanga, labda kama walitaka kupata moja kwa moha
kutoka kwa waandaaji.
“Kuhusu tarehe ya mashindano na vituo, Yanga wanafahamu na tumeshawatumia”. Alisema Mwesigwa.
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0 comments:
Post a Comment