Wakati jumuiya ya kimataifa inaziimarisha juhudi ili mapigano yasimamishwe katika Ukanda wa Gaza,Israel imesema asakari wake wamewaua wapiganaji 10 wa Hamas katika mapambano ya bunduki yaliyotokea mapema asubuhi leo. Kwa mujibu wa Israel wapiganaji hao wa Hamas walijaribu kujipenyeza ndani ya Israel kwa kupitia katika njia ya chini ya ardhi kwenye mpaka.
Obama atoa mwito wa kusimamisha mapigano
Rais Barack Obama pia ameurudia mwito juu ya kuyasimamisha mapigano mara moja katika mazungumzo yake ya simu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mapema leo, wakati ambapo Waziri wake wa mambo ya nchi za nje John Kerry akiwapo Mashariki ya Kati katika juhudi za kuyasimamisha mapigano.
Lakini Israel imeendelea na mashambulio leo. Watu tisa kutoka ukoo mmoja wameuawa kutokana na shambulio la ndege katika mji wa kusini wa Rafah. Saba kati ya waliouawa walikuwa watoto. Shambulio hilo lilitokea baada ya Wapalestina zaidi ya 150 kuuawa, hapo jana , yaani siku mbaya kabisa kwa Wapalestina tokea Israel ianze mashambulio siku 14 zilizopita.
Askari 18 wa Israel pia wameuawa
Kwa upande wake Israel imesema askari wake 13 waliauwa jana pekee ,ndani ya Ukanda wa Gaza na hivyo kuifanya idadi ya Waisraeli waliouawa tokea majeshi ya Israel yaingine katika Ukanda wa Gaza ifikie 18 .
Idadi ya Wapalestina waliouawa hadi leo Jumatatu ni zaidi ya 500 ukiwaondoa wapiganaji 10 waliojipenyeza ndani ya kusini mwa Israel.Askari wa Israel walipambana na Wapalesttina hao na kuwaua .Lakini askari kadhaa wa Israel pia walijeruhiwa.
Mjumbe wa Shirika la misaada la Umoja wa Mataifa aliepo ugani kwenye Ukanda wa Gaza Robert Turner pia metoa mwito wa kuyasimamisha mapambano mara moja.
Katibu Mkuu aongezea uzito sauti yake
Na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambae kwa sasa yuko katika Mashariki ya Kati katika juhudi za kuleta amani ameitaka Israel ijaribu kujizuia kwa sababu amesema watu wengi wasiokuwa na hatia wanakufa.
Katika kadhia nyingine jeshi la Israel limesema linayachunguza madai ya wapiganaji wa Wapalestina kwamba wamemteka askari mmoja wa Israel.Wapiganaji wa Hamas wamesema askari huyo anaitwa Shaul Aaron.
Mjumbe wa Wapalestina kwenye Umoja wa Mataifa Ryad Mansour ameilamu jumuiya ya kimataifa kwa kushidwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya Israel. Na Kiongozi wa Hamas Khaled Meshaal na Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mohmoud Abbas wanatarajiwa kukutana leo.
Mwandishi:Mtullya Abdu.afpe,rtre,
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman
0 comments:
Post a Comment