Jeshi
la Polisi Tanzania linapenda kutoa shukrani za dhati kwa wananchi wote,
vyama vya siasa, taasisi mbalimbali za serikali, madhehebu ya dini,
asasi za kiraia na vyombo vya habari kwa ushirikiano wa dhati katika
kusimamia masuala ya amani na usalama hapa nchini.
Tunapoelekea kipindi hiki cha
kusherehekea sikukuu ya Eid-El-Fitr, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa
wananchi wote kuwa makini na kusheherekea sikukuu hiyo kwa amani na
utulivu pasipo vitendo ama viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani.
Ikumbukwe kuwa, wananchi wenye
imani ya kiislam na hata madhehebu mengine hutumia muda huo kwenda
kuabudu pamoja na muendelezo wa sherehe hizo kwenye maeneo mbalimbali ya
starehe. Uzoefu umeonyesha kuwa baadhi ya watu hutumia kipindi hicho
cha sikukuu kama mwanya wa kufanya matukio ya uhalifu kutokana na
mikusanyiko hiyo ya watu.
Jeshi la Polisi linapenda
kuwaondoa hofu wananchi wote kuwa, limejipanga kikamilifu kuhakikisha
wananchi kote nchini wanasherekea sikukuu hiyo kwa amani na utulivu.
Ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya kuabudia, fukwe za bahari,
sehemu za starehe na maeneo mengine yote, aidha, tunapenda
kuwatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara, kuwa
makini kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani na hasa kwa madereva
wa magari na pikipiki kuepuka kwenda mwendo kasi na kutumia vilevi
wawapo kazini.
Katika kuhakikisha usalama kwenye
kumbi za starehe, wamiliki wa kumbi hizo wazingatie uhalali na matumizi
ya kumbi zao katika uingizaji wa watu kulingana na uwezo wa kumbi hizo,
badala ya kuendekeza tamaa ya fedha kwa kujaza watu kupita kiasi.
Jeshi la Polisi linapenda kuwashukuru wale wote ambao tayari
wamefunga kamera za CCTV katika maeneo yao ya starehe, hususani yale
yanayokuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu, yakiwemo maduka, hoteli na
maeneo ya benki. Aidha, Jeshi la Polisi linaendelea kuwasisitiza wale
ambao bado hawajaweka kamera hizo, kuweka ili ziweze kusaidia kubaini
wahalifu na hata kurahisisha ukamataji endapo uhalifu unatokea.
Vilevile, wazazi wawe makini na
watoto wao na hasa disko toto, ili kuepuka ajali na matukio mengine
yanayoweza kusababisha madhara juu yao.
Aidha wananchi wachukue tahadhari
watokapo kwenye makazi yao wasiache nyumba wazi ama bila mtu na watoe
taarifa kwa majirani zao, na pale wanapowatilia mashaka watu
wasiowafahamu wasikae kimya bali watoe taarifa haraka kwenye vituo vya
Polisi vilivyo karibu nao au kwa namba ya simu ifuatayo 0754 785557, ili
hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba – SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
0 comments:
Post a Comment