
Rais wa Simba sc, Evans Elieza Aveva jana amekabidhiwa rasmi kijiti cha kuiongoza klabu hiyo
RAIS wa Simba sc, Evans Elieza Aveva amekabidhiwa
rasmi kijiti cha uongozi na mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Ismail Aden Rage.
Makabidhiano hayo yalifanyika jana makao makuu ya
klabu hiyo, mtaa wa Msimbazi, Kariokoo, jijini Dar es salaam ambapo viongozi wa zamani
na wapya walikutana pamoja kwa ajili ya zoezi hilo muhimu.
Aveva na wenzake walikabidhiwa makaburasha yote na
Rage ikiwa ni kuashiria kuingia ofsini rasmi kuanza safari ndefu ya miaka minne
ya uongozi.
Nilisikiliza kwa umakini hutuba za viongozi wote
wawili,kwa maana ya aliyemaliza muda wake, Rage na rais mpya Aveva.
Katika hotuba ya Rage, niligundua busara kubwa ndani
yake. Kubwa ambalo nimeona lina maana kubwa ingawa yote yalikuwa na maana ni
kudumisha umoja katika klabu hiyo.
Kumbukumbu za Rage zilikuwa sahihi sana ambapo
alieleza kuwa wagombea wote wakati wanapiga kampeni zao kuelekea uchaguzi mkuu
uliofanyika juni 29 mwaka huu walisisitiza kudumisha umoja katika klabu hiyo.
Aveva alikuwa miongoni mwa wagombea waliosisitiza
kudumisha umoja na mshikamano katika klabu ya Simba sc.
Kama wagombea wote walikuwa wanazungumza jambo
hili, haihitaji muda na akili nyingi kujua kuwa Simba haikuwa na umoja kwa muda
mrefu.
Katika safari ya Rage, kuliibuka migogoro mingi ya
kiuongozi, hata wanachama walikuwa na matatizo na uongozi huo.
Mwenyekiti wa Simba aliyemaliza muda wake, Ismail Aden Rage
Mara kadhaa wanachama walithubutu kujaribu
kumpindua Rage, lakini majaribio yao yalishindikana kwa mujibu wa katiba. Hata
viongozi wengine walifanya majaribio ya kumpindua Rage ikiwemo Joseph Itang`are
`Mzee Kinessi`, lakini ilishindikana kwasababu mheshimiwa mbunge alilindwa na
katiba ya Simba.
Kutokana na hali hiyo ya kukosekana umoja, kila
mgombea aliingia kwa sera ya kurudisha umoja na mshikamano kama ilivyokuwa
miaka ya nyuma.
Rage kwa upande wake anatambua kabisa kuwa umoja
haukuwepo na ndio maana jana karudia maneno ya wagombea hao kama ishara ya
kuwakumbusha.
Alimuomba Aveva kumaliza tofauti zote na makundi
yote ikiwa ni pamoja na kuwasamehe wanachama 69 waliosimamishwa uanachama wao baada
ya kupeleka masuala ya klabu mahakama ya kawaida.
Rage alimwambia Aveva kuwa anaomba kufikia mkutano
mkuu utakaofanyika Agosti 3 mwaka huu awe amefikia maamuzi, hususani kutangaza
msamaha kwa wanachama hao.
Kundi la watu 69 ni kubwa sana, na kuna uwezekano
wapo wengine nyuma yao ambao hawakufika mahakamani. Kama Aveva ataamua
kupambana na kundi hili, basi suala la umoja litakuwa ndoto.
Kwa mujibu wa katiba ya Simba, TFF, CAF na FIFA,
ni marufuku masuala ya mpira kupelekwa katika mahakama za kawaida za haki.
Ukifanya hivyo unajifungia mwenyewe katika masuala ya mpira.
FIFA wanataka masuala yote ya mpira yatatuliwe
kwenye mfumo wake wa sheria na si vinginevyo.
Michael Richard Wambura alienguliwa mara mbili katika uchaguzi wa Simba na suala lake lilizua mvutano mkubwa
Rage alikiri kuwa Aveva yupo sahihi kuwasimamisha
wanachama hao na hajavunja katiba ya Simba.
Ni kweli, hatua alizochukua Aveva ni sahihi wala
hakuna tatizo. Lakini kuna busara inatakiwa kutumika kwasababu mambo ya
uchaguzi siku zote yanakuwa na mambo mengi.
Kutofautiana ni kawaida. Walienda mahakamani,
yawezekana walikuwa na hoja na ndio maana mahakama ilikubali kufungua shauri
lao, lakini bado si suala la kulifumbia macho.
Wenzetu Nigeria wameshafungiwa na FIFA baada ya
serikali kuingilia masuala ya mpira. Hatupendi kuona klabu wala TFF inafikia
huko.
Umoja ni nguzo ya kuifanya Simba iwe imara. Aveva
anatakiwa kuifanya Simba iwe moja. Ameingia rasmi madarakani hapo jana, ni
jambo la msingi kuanza kila kitu upya.
Migongano yote iliyotokea kwenye uchaguzi
inatakiwa kumalizwa kwa busara. Kama itaendelezwe, basi tutegemee kuona makundi
tena.
Rage alisisitiza kuwa Aveva anatakiwa kuwasamehe
wanachama wote waliofanya makosa. Kwa maana hiyo hata Michael Richard Wambura
anastahili msamaha huo.
Wambura baada ya kusikia tamko la Aveva
kuwasimamisha wanachama 69 likiwemo na suala lake na kusema mkutano mkuu ujao
utajadili, alimuomba Aveva kusitisha suala hilo na kutoliendeleza kwasababu
litaivuruga Simba.
Kwa bahati mbaya aliongea Wambura, lakini mambo
aliyoongea Rage jana yanafanana sana na aliyosema katibu mkuu huyo wa zamani wa
FAT.
Baada ya maneno yote hayo, Aveva alimshukuru Rage
kwa ushauri huo na akaahidi kulifanyia kazi.
Akaenda mbali kwa kumpongeza Rage kwa kazi kubwa
aliyofanya akiwa kiongozi. Akakiri kuwa si jambo jepesi kuongoza klabu kubwa
kama Simba.
Mazuri yote ya Rage atayaendeleza ikiwemo suala la
Uwanja huko Bunju. Yalikuwa maneno mazuri sana kutoka kwa `Mr. Presidaa` wa
Simba.
Kulifanyia kazi alikosema Aveva, binafsi naamini
itakuwa ni kuwasamehe. Hiyo ndio busara ninayotegemea kutoka kwa rais huyo wa kwanza
katika historia ya Simba.
Si jambo la kupuuza hata kidogo. Ushauri wa Rage
ulikuwa mzuri mno. Kuwatenga watu 69 ni jambo baya, yawezekana wakawa zaidi ya
hao.
Busara ni kuwasamehe na kuwarudisha kundini kwa
amani ili simba ianze kujengwa upya.
Kuendeleza haya, basi sinema zitaendelea kuonekana
ndani ya klabu hiyo na matokeo yaliyopatikana kwa miaka mitatu mfululizo
hayatakwepeka.
Aveva kazi kwako, Simba ni yako na wewe ndiye
kiongozi wa juu zaidi. Jaribu kulitafakari kwa kina ili maamuzi utakayotoa yawe
chanya kwa Simba.
Rage hakuwa mbaya kwa kila kitu. Yeye ni binadamu,
kukosea ni kawaida kama ilivyo kwa mtu yeyote, lakini ana mazuri mengi, hayo inabidi
Aveva apambane nayo kuyaendeleza.
Ni uungwana kuheshimu kazi aliyofanya mwenzako,
madhaifu huwa hatusemi kwasababu ndio mambo unatakiwa kuyarekebisha.
Umoja haukuwepo wakati wa Rage, huo ulikuwa udhaifu,
sasa Aveva ndiye mtu wa kufuta hilo na kuweza kufanya kazi hiyo, hawa watu 69
wanatakiwa kufikiriwa kwa mtazamo chanya.
Kila la kheria wekundu wa Msimbazi Simba katika kuijenga klabu yenu.
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
0 comments:
Post a Comment