WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa
ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu yanaendelea japo kwa kiasi
kikubwa hatma yake inategemea kukamilika kwa mchakato wa Katiba mpya.
Ametoa kauli hiyo leo
mchana (Jumatatu, Juni 30, 2014) wakati akizungumza na Mameya wa Majiji,
Manispaa na Wenyeviti wa Halmashauri za Miji na Wilaya Tanzania katika
kikao cha siku moja kilichofanyika kwenye ukumbi wa Regal Naivera jijini
Tanga.
Waziri Mkuu yuko Tanga
kwa ajili ya sherehe za Serikali za Mitaa ambayo kilele chake
kitafanyika kesho Julai mosi kwenye uwanja wa Tangamano jijini hapa.
Ameamua kukutana na viongozi hao ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya
kukutana nao aliyoitoa Mei 14, 2014 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa
ALAT.
“Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa bado ni kitendawili kwa sababu kwa kiasi kikubwa inategemea sana
kukamilika kwa Mchakato wa Bunge la Katiba,” alisema na kuongeza:
“Kama Wizara tunaendelea
na maandalizi tukiamini uchaguzi upo, kama hiyo fursa isipotokea bado
tutakuwa tumekamilisha maandalizi kwa upande wetu.Tunaendelea kuandaa
kanuni kwa kushirikisha wadau wote,” alisema.
Waziri Mkuu alitumia
fursa hiyo kusisitiza suala la ukusanyaji mapato na udhibiti wa matumizi
ya fedha za Serikali. Kuhusu mapato, Waziri Mkuu alisema katika mwaka
wa fedha wa unaoisha sasa, hali ya ukusanyaji mapato haikuwa nzuri.
Kufuatia hali hiyo,
Waziri Mkuu alisema amewaandikia barua Wakuu wa Mikoa akiwataka waweke
utaratibu wa kutoa taarifa kila baada ya miezi mitatu juu ya makusanyo
ya kila Halmashauri zilizo kwenye mikoa yao.
“Katika taarifa hizi
itabidi kila Halmashauri ieleze ilipanga kukusanya kiasi gani, je
imefikia lengo na kama sivyo ni kwa nini. Nia yetu ni kutrack down
makusanyo na kuona yamekwama wapi na yamekwamishwa na nini,” alisema.
Kuhusu udhibiti wa
matumizi, Waziri Mkuu aliwataka Mameya na Wenyeviti hao kuendelea
kuwabana wahusika ili kudhibiti matumizi yasiyofaa. “Lazima muendelee
kuwabana na kuwasimamia wakurugenzi na wataalaam wa kwenye Halmashauri
zenu. Fanyeni kazi kwa ufanisi, msiwachekee wale wanaoharibu,”
aliongeza.
“Ili muweze kuwabana
vizuri, ni lazima mdai kupatiwa taarifa za fedha kutoka kwa Mkaguzi wa
Ndani (Internal Auditor)… kuna baadhi ya watendaji wanadai kuwa hizi
taarifa ni siri wakati siyo siri,” alisema.
Aliwaeleza washiriki wa
kikao hicho kwamba taarifa hizo ni muhimu kwao kuzipata na zitawasaidia
kuonyesha mapungufu yoyote kama yapo.
Aliwataka kila mmoja wao kwa nafasi zao za Meya na Mwenyekiti wahakikishe wanalenga kupandisha pato la wananchi wanaowaongoza.
0 comments:
Post a Comment