WASHINDI wa tatu wa ligi kuu soka Tanzania bara
msimu uliopita, klabu ya Mbeya City fc imeanza zoezi la kutafuta wachezaji
wapya watakaosajiliwa kwa ajili ya kikosi cha pili.
Akizungumza na mtandao huu leo mchana, katibu mkuu wa klabu hiyo, Emmanuel Kimbe amesema kuwa wachezaji
wanaotakiwa ni kuanzia miaka 17 hadi 22 na zoezi hilo limeanza juzi na
litafikia tamati juni 30 mwaka huu.
“Sasa hivi shughuli inayoendelea ni kufanya utambuzi
wa baadhi ya wachezaji, lakini ni wachezaji wadogo wadogo wenye miaka 17 mpaka
22. Zoezi limeanza jana (juzi) saa tano litakwenda mpaka tarehe 30. Nia ni
kupata wacheza watakaocheza kikosi cha pili na baadaye kikosi cha kwanza”. Alisema
Kimbe.
Kimbe aliongeza kuwa baada ya zoezi hilo
watakutana pande mbili za utambuzi kwa maana ya viongozi na benchi la ufundi
ili kukamilisha usajili wa makinda hao.
Kuhusu asajili mwingine, Kimbe alisema utaendelea,
lakini wanatarajia kusitisha kwasababu kwa kiasi kikubwa wachezaji wote
wamebakia kikosini.
Kimbe alisema kwamba kikosi cha Mbeya City chini
ya kocha bora wa msimu uliopita, Juma Mwambusi kitaingia kambini kuanzia julai
15 mwaka huu.
Hata hivyo aliongeza kuwa wanatarajia kucheza
mechi za kirafiki nje ya nchi ili kujiweka sawa kwa msimu mpya unaotarajia
kuanza kushika kasi mwezi agosti mwaka huu.
Msimu uliopita, Mbeya City ilimaliza nafasi ya
tatu kwa kujikusanyia pointi 49 katika mechi 26 ilizocheza.
City ilishinda mechi 13, sare 10 na kufungwa mechi
tatu dhidi ya Yanga sc, Coastal Union na mabingwa Azam fc.
Kikosi hicho cha Mwambusi kilitikisa nyavu mara 33
na nyavu zake kuguswa mara 20.
Licha ya matokeo hayo, Mbeya City iliifanya ligi
kuu kuwa maarufu zaidi kutokana na ubora wake wa uwanjani na namna mashabiki wa
soka wa jijini Mbeya walivyoungana
kuisapoti timu yao.
Timu mbili zilizopanda na Mbeya City, Rhino
Rangers na Ashanti United zilishindwa kuhimili mitanange ya ligi kuu na kushuka
daraja.
Mbali na timu hizo, nao maafande wa JKT Oljoro
walishuka daraja na kuzipisha timu za Stand United ya Shinyanga, Ndanda fc ya
Mtwara na Polisi Morogoro ya Mkoani Morogoro.
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0 comments:
Post a Comment