KITUO cha Usuluhishi (CRC)
kinachofanya kazi chini ya Chama cha Wanahabari Wanawakecha (TAMWA)
kimejipanga kutoa elimu kwa jamii kuhakikisha kinapambana na matumizi ya
pombe kupindukia kwa jamii suala ambalo limezidisha vitendo vya ukatili
wa jinsia unaofanywa na watumiaji pombe kupindukia.
Akizungumza na wahariri wa habari
jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Valerie Msoka
alisema utafiti uliofanywa na Shirika la IOGT International unaonesha
kuwa kiwango cha unywaji pombe jijini Dar es Salaam ni asilimia 47.6 kwa
wanaume na asilimia 29 kwa wanawake huku ikibainika kuwa kuna uhusiano
mkubwa kati ya vitendo vya ukatili na matumizi ya pombe kupita kiasi.
Bi. Soka alisema takwimu
zinaonesha kuwa wanawake ambao waume zao wanalewa mara kwa mara wengi
wao wanakumbana na ukatili unaohusisha vipigo, kuumizwa na ukatili wa
kingono kwa asilimia 77, huku kiwango cha ukatili kwa wanawake ambao
waume ama wenzi wao hawanywi pombe ni asilimia 33.
“…Utafiti uliofanywa na shirika la
IOGT International unaonyesha kwamba kiwango cha unywaji pombe katika
jiji la Dar es Salaam ni asilimia 47.6 kwa wanaume na asilimia 29 kwa
wanawake…lakini takwimu kutokana na utafiti wa Demographia na Afya
Tanzania (TDHS) 2010…unaonesha wanawake ambao waume zao wanalewa mara
kwa mara wengi wao wanakumbana na ukatili unaohusisha kipigo/kuumizwa na
ukatili wa kingono kwa asilimia 77,” alisema.
Aidha aliviomba vyombo vya habari
kushirikiana na TAMWA kutoa elimu kwa jamii kupunguza matumizi ya pombe
kupindukia kwani licha ya ukatili huo familia pia zimekuwa zikiathirika
kiuchumi juu ya matumizi ya pombe huku baadhi ya watoto wakikosa huduma
za msingi kutoka kwa baadhi ya wazazi ambao ni walevi kupindukia.
Alisema TAMWA inatekeleza mradi wa
kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana unaosababishwa na
pombe huku lengo kuu ikiwa ni kuhakikisha maisha ya wanawake na watoto
yanaboreshwa kwa kuimarisha sheria na kupunguza ukatili wa kijinsia
unaosababishwa na unywaji wa pombe kupindukia.
Hata hivyo alisema tayari chama
hicho kimeanza kufanya utafiti mwingine katika Wilaya ya Kinondoni
kuangalia madhara yanayotokana na unywaji wa pombe kupindukia ili
kuangalia hali halisi ya matumizi ya pombe eneo hilo na madhara ambayo
yamekuwa yakitokana na matumizi hayo.
Alisema malengo mengine ya mradi
ni pamoja na kuboresha maisha ya wanawake na watoto kwa kuimarisha
sheria na kupunguza ukatili wa kijinsia unaosababishwa na unywaji wa
pombe katika wilaya ya Kinondoni na pia kujenga uelewa miongoni mwa
jamii juu ya madhara yatokanayo na unywaji wa pombe kupindukia.
Mkurugenzi huyo Mtendaji wa TAMWA
aliongeza kuwa mapambano hayo pia yatasaidia, kukabiliana na matumizi ya
pombe na kutoa taarifa kwa vyombo husika kuhusu ukatili dhidi ya
wanawake unaotokana na matumizi ya pombe, ikiwa ni pamoja na kujenga
uwezo wa jamii kukabiliana na ukatili unaosababishwa na unywaji wa pombe
dhidi ya wanawake na watoto.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
0 comments:
Post a Comment