FIFA
imethibitisha kuwa Uruguay imekata Rufaa kwao kupinga kufungiwa kwa
Straika wao Luis Suarez kwa kosa la kumuuma Meno Mchezaji wa Italy
Giorgio Chiellini wakati wa Mechi ya Kombe la Dunia huko Brazil.
Uamuzi wa kukata Rufaa ulipelekwa FIFA Jana na Chama cha Soka cha Urguay.
Mkuu wa Habari wa FIFA, Delia Fischer,
amesema: “Tumepokea azimio toka Uruguay kwamba watakata Rufaa.
Walituambia Jana jioni. Sababu za kukata Rufaa zinatakiwa ziwasilishwe
kwa maandishi ndani ya Siku 7.”
Suarez amefungiwa na FIFA Miezi minne
kutojihusisha na chochote kuhusu Soka ikiwemo kutokanyaga Mazoezi na
kutoingia Uwanja wowote wa Mpira na pia kutocheza Mechi 9 za Kimataifa
za Uruguay pamoja na kupigwa Faini ya Dola 111,000.
Wakati huo huo, Barua ya Suarez
iliyowasilishwa kwa Kamati ya Nidhamu ya FIFA kama utetezi wake kwa kosa
hilo la kumuuma Meno Chiellini imedai hakumuuma Meno ila aliteleza na
kumwangukia Mpinzani wake.
Barua hiyo imesema: “Haikutokea kama
mlivyoeleza kwamba nilimuuma au nilikusudia kumuuma…..Niliteleza na
kumwangukia Mpinzani wangu. Uso wangu ukamgonga na kuaacha mchubuko
shavuni kwangu na maumivu makali kwenye Jino langu.”
Hata hivyo, Jopo la Watu 7 la Kamati ya
Nidhamu ya FIFA liliukataa utetezi huo na kuamua kuwa aliuma ‘akiwa na
nia, makusudi na bila kuchokozwa.’
Pia Jopo hilo lilithibitisha kuwa Refa
wa Mechi hiyo, Marco Rodriguez wa Mexico na Wasaidizi wake wawili,
hawakuliona tukio hilo kwa vile Mpira ulikuwa eneo jingine wakati huo.
Jopo hilo la Kamati ya Nidhamu ya FIFA
lilikuwa chini ya Mwenyekiti, Claudio Sulser, Mchezaji wa zamani wa
Kimataifa wa Switzerland, akisaidiwa na Wajumbe kutoka Cook Islands,
Hong Kong, Pakistan, Panama, South Africa na Singapore.
0 comments:
Post a Comment