Saturday, 28 June 2014

HOSPITALI YA MUFINDI YAPATA MSAADA WA VITI VYA KUBEBA WAGONJWA

dddd  
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Goodluck Mlimbila alikijaribu kusukuma moja kati ya viti 33 vilivyotolewa na asasi ya MUVIMA kwa ajili ya hospitali ya wilaya ya Mufindi. Anayefurahi katikati ni mkurugenzi mwenza wa MUVIMA, Albert Chalamila akipongezwa na Katibu wa Afya wa Wilaya hiyo, Atupekisye Mwakifamba IMG_0157 
Albert Chalamila na baadhi ya wanahabari wakiangalia hali ilivyo ndani ya wodi ya wazazi ya hospitali hiyo; hapa wanaonekana baadhi ya wajawazito wanaolala chini kutokana na ukosefu wa vitanda.
Na Denis Mlowe,Mufindi
 
ASASI ya Mufindi Vijana kwa Maendeleo (MUVIMA) imetoa msaada kwa hospitali ya wilaya ya Mufindi yenye matatizo mbalimbali  kwa lengo la kusaidia kutoa huduma bora kwa kutoa viti 33 vya kubeba wagonjwa.
Akikabidhi msaada huo hivi karibuni Kaimu Mkurugenzi wa MUVIMA, Albert Chalamila alisema asasi yao imeguswa na kero mbalimbali zinazoikabili hospitali hiyo na kwa kuanzia ililazimika kutafuta viti hivyo kwa lengo la kusaidia hospitali hiyo yenye matatizo mbalimbali  yanayofifisha utoaji wa huduma bora za afya, zikiwemo zile za wajawazito na watoto,
 
Alisema kwa msaada wa asasi ya kimataifa ya Rafiki Surgical Mission ya Australia waliomba msaada huo baada kuomba msaada wa vitanda kwa ajili ya hospitali hiyo hivyo vitanda 23 vimekwishawasili bandari ya Dar es Salaam na tumeanza na viti vya kubeba wagonjwa.
 
Alisema Mkurugenzi Mkuu wa MUVIMA, Cosato Chumi anaendelea na utaratibu wa kuvitoa vitanda hivyo bandarini na mara baada ya shughuli hiyo kukamilika vitakavifdhiwa kwa uongozi wa hospitali hiyo.
 
Kaimu Mganga wa Hospitali ya Wilaya ya Mufindi, Dk Goodluck Mlimbila kwamba vitapunguza adha waliyokuwa wanapata watoa huduma wa hospitali hiyo ya kupokea na kubeba mikononi, wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.
 
Akishukuru kwa msaada huo, Dk Mlimbila alisema hospitali hiyo ina upungufu mkubwa wa vifaa tiba na dawa na akalitaja eneo lenye tatizo zaidi kuwa ni lile la huduma kwa mjamzito na watoto.
 
Alisema katika kuboresha huduma za uzazi, jengo lenye uwezo wa kulaza wajawazito zaidi ya 100 na lenye chumba cha upasuaji na kile cha kuhifadhia watoto wanaozaliwa kabla ya muda lilijengwa katika hospitali hiyo ambayo awali ilikuwa ikitumia jengo lenye uwezo wa kuweka vitanda 27 tu.
 
Alisema msaada uliotolewa na MUVIMA una umuhimu mkubwa katika hospitali hiyo kwani utarahisisha huduma za ubebaji wagonjwa kutoka eneo moja hadi lingine na utapunguza idadi ya wajawazito wanaolala chini baada ya vitanda vilivyoahidiwa kuwasili.
 
Naye Katibu wa Afya wa wilaya hiyo, Atupakisye Mwakifamba aliwataka MUVIMA na wadau wengi kujitokeza kuzimaliza kero za utoaji huduma zinazoikabili hospitali hiyo na vituo vingine vingi vya huduma wilayani humo.
 
Mwakifamba alisema pamoja na wilaya hiyo kuwa na idadi ya kuridhisha ya watoa huduma wenye ujuzi, inakabiliwa na upungufu mkubwa wa vifaa tiba, dawa na magari ya kubeba wagonjwa.

0 comments: