Monday, 30 June 2014

LOUIS VAN GAAL KUMBADILI RVP KWENYE MECHI, NI SALAMU SPESHO MAN UNITED!


LVG-RVPWACHAMBUZI huko Uingereza wametafsiri kuwa kumbadili Nahodha wa Netherlands Robin van Persie wakati Holland iko nyuma kwa Bao 1-0 walipocheza na Mexico ni ujumbe tosha toka kwa Louis van Gaal kwa Klabu yake mpya Manchester United kuwa hatakuwa na masihara akianza rasmi kibarua chake.
Akizungumzia kumtoa Robin van Persie, ambae ni Nahodha na ndie Mfungaji wao mkuu, huku wakiwa nyuma kwa Bao 1-0 na Dakika zikiwa zimebaki 10, Louis van Gaal, ambae ndie Kocha wa Holland, ameeleza: “Kumbadili ni kubadili mbinu. Tusisahau yeye alijiunga na Timu akitokea kwenye Majeruhi. Ni ngumu kwake kucheza Dakika 90 katika hali ya Joto kama lile.”
Wakati akitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Klaas Jan Huntelaar ambae ndie aliefunga Bao la ushindi kwa Penati ya Dakika ya 94, Van Persie alioonyesha alikuwa mchovu ikiwa ni wazi Joto lilimmaliza.
Hata Meneja wa Mexico, Miguel Herrera, alikiri Joto liliathiri uchezaji kwa kusema: “Hatukuona Mechi nzuri. Hata Timu nzuri kama Netherlands inaathirika kwa Joto -hamna kasi, uchezaji hupungua!”
Alipomwingiza Klaas Jan Huntelaar, Louis van Gaal ilibidi abadilishe Mfumo kwa mara ya 3 kwenye Mechi hiyo kwani alianzia 5-3-2 kwenda 4-3-3 na zikibaki Dakika 10 huku wakiwa nyuma 1-0, alitumia 4-4-2 na kuwatumia Klaas Jan Huntelaar na Dirk Kuyt kama Mastraika wawili mbele.
Van Gaal ameeleza: “Tulikuwa na Mapumziko ya kujipoza, kunywa Maji na hapo niliweza kuanza na Mpango B na kuwaambia wote. Tumefanyia mazoezi kuwatumia Huntelaar na Kuyt kama Mastraika na kutumia Mipira mirefu. Baada ya kusawazisha nilimrudisha Kuyt kucheza Fulbeki na tukatumia 4-3-3 kwa mara nyingine. Hapo ndipo tukawa tunampata Robben mara nyingi na ndio maana akalazimisha Penati.”
Wachambuzi wanadai ni wazi maamuzi kama hayo yategemewe na Wachezaji wa Man United Msimu ujao.
Mifumo itabadilika, uchezaji utabadilika kufuatana na Mechi yenyewe na hakuna Mtu atakayepona kubadilishwa hata kama Staa namna gani.
Akijibu swali kwa nini alimbadila Van Persie, Van Gaal alisisitiza: “Kocha huyu anataka ushindi. Ndio maana amefanya mabadiliko. Hamna ugumu zaidi ya hilo.”

0 comments: