Felix Mwagara
SERIKALI
imewapa uraia wa Tanzania Wakimbizi wa Kisomali wenye asili ya Kibantu
1,514 waliokuwa wanaishi katika Makazi ya Chogo, Wilaya ya Handeni
mkoani Tanga.
Wakimbizi
hao ambao walikimbia nchi yao Somalia baada ya vita kutokea mwaka 1990
ambapo baadhi yao 3,000 walikimbilia nchini kwa kutambua kuwa ndipo
mababu zao walikotoka, Serikali iliwapokea na kuwahifadhi katika Kambi
ya Mkuyu iliyopo Mkoani Tanga ambapo walikuwa wakipata msaada kutoka
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR).
Akizungumza
jana baada ya kuwapa vyeti vya uraia wakimbizi hao ambao kwasasa ni
raia halali wa Tanzania, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias
Chikawe alisema wakimbizi hao walihamishwa na Serikali mwaka 2003 kutoka
Kambi ya Mkuyu kuja katika Makazi ya Chogo ili wapatiwe mashamba kwa
ajili ya kujishughulisha na kilimo ili waweze kujitegemea.
“Nachukua
nafasi hii kuwapongeza wote waliopewa uraia wa Tanzania, wajisikie kuwa
wao ni raia huru sawa na Watanzania wengine. Hata hivyo nawasihi muwe
waadilifu na watiifu kwa sheria zote za Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania,” alisema Chikawe.
Chikawe
pia alitoa pongezi kwa UNHCR kwa kujenga miundombinu muhimu katika
makazi hayo ya Chogo na pia kuwawezesha wakimbizi hao kuishi maisha ya
kujitegemea wenyewe kabla hata ya kuwa raia.
Hata
hivyo, Waziri Chikawe aliwataka wakimbizi 150 katika makazi hayo ya
Chogo ambao hawakuomba kuwa raia wa Tanzania kwa nia ya kurudi nchini
Somalia pale hali ya amani itakapopatikana wanapaswa kuendelea kutii
sheria za nchi zinazotawala hifadhi ya ukimbizi nchini.
Aidha,
Mwakilishi Mkazi wa UNHCR, Joyce Mends-Cole katika hafla hiyo
aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwapa uraia wakimbizi hao na
Shirika lake litaendelea kutoa misaada mbalimbali kwa wakimbizi
waliobaki katika makazi hayo pamoja na sehemu nyingine nchini.
Hafla
hiyo ya ugawaji wa vyeti vya uraia ilihudhuriwa na Maofisa wa Idara ya
Wakimbizi na Uhamiaji zilizopo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mwakilishi wa Mkuuu wa Mkoa wa Tanga na Serikali ya Kijiji cha Chogo
pamoja na Maofisa wa UNHCR
0 comments:
Post a Comment