Wednesday, 16 April 2014

MSIMU HUU YANGA INAWAZIDI SIMBA KWA KILA KITU , NINI KITATOKEA JUMAMOSI?

DSC_0019


Na Baraka Mpenja, Dar Es Salaam
0712461976
SIMBA SC watakabiliana na Yanga katika mechi ya kufunga pazia la ligi kuu soka Tanzania bara jumosi ya wiki hii kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Timu hizi zitakutana zikiwa na mafanikio tofuati msimu huu ambapo Yanga wameambulia nafasi ya pili, huku Mnyama akijikongoja katika nafasi ya nne.
Simba na Yanga zinapokutana katika mechi za ligi au mashindano mengine, wachezaji, mabenchi ya ufundi, viongozi na mashabiki wa klabu hizi kongwe nchini wanakuwa katika presha kubwa.
Unapozungumzia historia ya soka la Tanzania, ni dhambi kubwa kutozitaji klabu hizi mbili zenye mashabiki kila kona ya nchi hii.
Mengi yanatokea kila mechi zao zinapokaribia. Wachezaji mara nyingi wanasakiziwa kuuza mechi pale timu moja inapofungwa.
Wakati mwingine inasemekana viongozi wa timu hizi huenda kwa waganga wa kienyeji kwenda kuroga timu pinzani.
Suala la ushirikiana linazungumzwa sana katika klabu hizi, lakini ni jambo gumu kulithibitisha kisayansi kama kweli linafanya kazi.
Simba na Yanga zinakutana jumamosi, huku Yanga wakiwazidi wenzao kwa kila kitu.
Yanga wamecheza mechi 25 sawa na Simba sc, lakini wameweza kushinda mechi 16, kutoa sare 7 na kufungwa mechi 2 tu, hivyo kufikisha pointi 55 katika nafasi ya pili.
Pia Yanga ndio klabu iliyofunga mabao mengi zaidi mpaka sasa ambapo imetikisa nyavu za timu pinzani mara 60, lakini wamefungwa mabao 18 na kuwa timu ya pili kufungwa mabao machache.
Mabingwa watetezi Azam fc wamefunga mabao 50 na kufungwa mabao 15 tu, hivyo kuwa timu yenye rekodi ya kufungwa mabao machache zaidi msimu huu.
Ukirejea kwa upande wa Simba sc, msimu huu upepo mbaya umevuma kwa upande wao kwasababu mpaka sasa wamecheza mechi 25 na kushinda mechi 9, sare 10 na kufungwa mechi 6.
Pia Mnyama Simba amefanikiwa kufunga mabao 40  na kuruhusu nyavu zake kuguswa mara 26.
Kwa takwimu hizi utagundua kuwa Yanga wamekuwa bora kwa kila kitu dhidi ya Simba sc.
Safu ya Ulinzi ya Yanga inayoongozwa na Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadri Haroub Canavaro, Kelvin Yondani na wengineo imekuwa bora zaidi ya Simba inayoongozwa akina William Lucian ‘Gallas’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ Joseph Owino, Donald Mosoti, Nassor Masoud ‘Chollo’ na wengineo.
Kigezo cha pekee ni idadi ya mabao ambayo mabeki wa timu zote wameruhusu kutikisa nyavu.
Yanga wamefungwa mara 15 na Simba mara 26, hivyo Yanga wamekuwa na beki imara zaidi ya watani zao.
Ukija safu ya ushambuliaji baina ya timu hizi, kuna utofauti mkubwa.
Yanga wamekuwa na makali zaidi baada ya kufunga mabao 60 mpaka sasa dhidi ya mabao 40 ya Simba sc.
Safu ya ushambuliaji ya Yanga haimtegemei mchezaji mmoja kwasababu wote Saimon Msuva, Mrisho Ngassa, Didier Kavumbagu, Jeryson Tegete, Hussein Javu, Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza wanaweza kufunga pale wanapopewa nafasi ya kucheza.
Washambuliaji wa Yanga ndio wanaoongoza kufunga mabao mengi zaidi na kuweka rekodi ya kufunga mabao mengi kuliko klabu yoyote katika mechi moja msimu huu.
Rekodi hii waliweka baada ya kuwafunga mabao 7-0 Ruvu Shooting ndani ya uwanja wa Taifa.
unnamed (10)Ukija upande wa Simba, mabao mengi yametengenezwa kupitia kwa nyota wao, Mrundi Amis Tambwe, japokuwa kuna wachezaji wengine kama akina Zahor Pazzi, Ramadhani Singano, Haruna Chanongo ambao wamekuwa wakifunga mara kadhaa.
Hata rekodi ya kushinda na kufungwa, Yanga wanawazidi Simba kwasasa wamefungwa mechi mbili tu wakati Simba wamechezea kichapo mara sita.
Kwa kuangalia takwimu hizi, unaweza kusema Yanga wana uwezo mkubwa wa kuwafunga Simba sc jumamosi, lakini mechi ya watani wa jadi ni kitu kingine.
Mzunguko wa kwanza, Yanga walikuwa bora zaidi ya Simba iliyosheheni wachezaji wengi vijana chini ya aliyekuwa kocha mkuu Abdallah Kibadeni `King Mputa`.
Kipindi cha kwanza Yanga walifunga mabao 3-0 na kujiamini kuwa wangeweka rekodi ya kuwafunga mabao mengi Simba na kulipa kisasi cha kuwahi kufungwa mabao 5-0.
Hata hivyo mambo yalikuwa tofauti kipindi cha pili ambapo Simba walikuja juu na kusawazisha mabao yote matatu na kutoa sare ya 3-3.
Haya yalikuwa moja ya matokeo ya ajabu baina ya klabu hizi.
Baada ya mechi hiyo,  timu hizi zilikutana tena desemba mwaka jana kwenye mechi ya `Nani Mtani Jembe` na kushuhudia Yanga iliyokuwa bora ikifungwa mabao 3-1.
Matokeo hayo yaliondoka na kocha mkuu Ernie Brandts na msaidizi wake Fredy Minziro waliofungashiwa virago.
Kuelekea katika mechi ya jumamosi, bado Yanga wanaonekana kuwa bora zaidi ya Simba.
Lakini Simba wameenda kuweka kambi Zanzibar na bila shaka watarejea na nguvu ya kuwavaa watani zao wa jadi.
Mpira wa miguu huwa ni mchezo wa hesabu, ukikosea kuzifanya basi unafungwa.
Ni kawaida kuona timu bora inafungwa na timu ya kawaida kama ilivyotokea kwa Yanga na Mgambo au Simba na Ashanti United.
Ukiangalia vikosi vya timu zote mbili, Yanga wana wachezaji wakali kuliko Simba, lakini si sababu ya kusema watashinda mechi.
Simba uliowaona katika mchezo uliopita na Ashanti si wale utakaowaona siku ya jumamosi.
Bila shaka wataingia kwa morali kubwa ya kutaka kushinda, na viongozi wao wamewataka wachezaji kuwafunga mahasimu wao ili kujipunguzia maumivu.
Usije kushangaa yanatokea matokeo ambayo watu wengi hawatarajii.
Mechi ya watani ina mambo mengi na si rahisi kutabiri kwa kuangalia vikosi vya vyao.
Usije ukaliwa nyumba yako, Mke wako, pesa zako kwa kuweka mzigo mezani na kutabiri matokea.
Usilete mchezo na mechi ya watani wa jadi, huwa timu zinacheza kwa kujituma mno.
Kila la kheri Simba na Yanga katika mechi yenu ya jumamosi

0 comments: