TAIFA STARS KWENDA ADDIS ABABA LEO
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imeondoka
jana(Mei 26 mwaka huu) usiku kwenda Addis Ababa, Ethiopia ambapo itaweka kambi
na kucheza mechi moja ya kirafiki kabla ya kwenda Morocco.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro
Premium Lager imeondoka saa 5 usiku kwa ndege ya EgyptAir ikiwa na kikosi cha
wachezaji 21 chini ya nahodha wake kipa Juma Kaseja.
Timu hiyo ikiwa Ethiopia, Juni 2
mwaka huu itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan ambapo siku inayofuata
itaondoka kwenda Marrakech, Morocco kwa kupitia Cairo, Misri. Mechi hiyo ya
mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji Morocco itachezwa Juni 8 mwaka huu
jijini Marrakech.
Mbali ya nahodha Kaseja, wachezaji
wengine wanaoondoka katika kikosi hicho ambacho kina wiki sasa tangu kingie
kambini jijini Dar es Salaam ni Mwadini Ally na Ally Mustafa ambao wote ni
makipa.
Wengine ni Shomari Kapombe, Kevin
Yondani, Aggrey Morris, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho
Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco,
Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd na Haruni Chanongo.
Wachezaji Mbwana Samata na Thomas
Ulimwengu ambao wako na timu yao ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo watajiunga moja kwa moja na Stars jijini Marrakech, Juni 4 mwaka huu
wakitokea Maputo, Msumbiji mara baada ya mechi yao ya Kombe la Shirikisho dhidi
ya Liga Muculumana ya huko.
Katika msafara huo wa Ethiopia
benchi la ufundi la Stars linaundwa na Kim Poulsen (Kocha Mkuu), Sylvester
Marsh (Kocha Msaidizi),Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Tasso (Meneja
wa timu), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari), Frank Mhonda (Mtaalamu wa
tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment