Monday, 20 May 2013

WAZABUNI MARA WAITISHA SERIKALI

Wazabuni Mara waitisha serikali

na Mwandishi wetu, Musoma

WAZABUNI wa ndani katika Mkoa wa Mara wameanza taratibu za kuifikisha serikali mahakamani kwa madai ya kushindwa kuwalipa deni lao linalodaiwa kufikia kiasi cha sh bilioni mbili. Kiasi hicho kinatokana na huduma mbalimbali zilizotolewa na wazabuni wa ndani kwa Magereza, vyuo vya ualimu na vyuo vya uganga vilivyopo mkoani Mara.
Akizungumza na Tanzania Daima, Mwenyekiti wa wazabuni mkoani Mara, Edward Muhere, alisema deni hilo ni kuanzia mwaka 2009 hadi sasa.
Alibainisha kuwa kwa hali ilivyo hivi sasa, serikali imeshindwa kuonesha nia ya dhati kulipa deni hilo hivyo wazabuni wameamua kufanya mchakato wa kuipeleka mahakamani.
Alisema kuwa kutokana na wazabuni hao kutolipwa kwa kipindi kirefu, baadhi yao wamefilisika na wengine kuuziwa mali zao baada ya kushindwa kulipa madeni waliyoyakopa kwenye taasisi za kifedha.
“Hivi hii serikali sikivu kwa akina nani hasa? Sisi wazabuni tulionesha uzalendo wa hali ya juu wa kutoa huduma kwa mkopo kwa serikali yetu, lakini leo haitulipi haki zetu kama wanavyolipwa wazabuni wa nje. Tumevumilia vya kutosha, sasa tumechoka, ngoja twende mahakamani,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema wamekubaliana kusitisha kutoa zabuni kwa taasisi hizo ili kuhakikisha serikali inawatendea haki wazabuni wa ndani kama inavyowatendea wa nje ya nchi.

0 comments: