Monday, 20 May 2013

WANANCHI WAPINGA ZIARA YA MADIWANI KYELA MBEYA

Wananchi wapinga ziara ya madiwani

BAADHI ya wananchi wilayani Kyela wamelalamikia ziara ya madiwani kwenda mkoani Dodoma kusikiliza bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa kusema ni ufujaji wa fedha za wananchi.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki, wananchi hao walidai madiwani hao walialikwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe kwenda kusikiliza bajeti hiyo kwa ufadhili wake, lakini wanashangaa kitendo cha Halmashauri ya Kyela kumsainisha sh milioni 1.66 kila diwani kwa ajili ya safari hiyo.
Walisema kutolewa kwa fedha hizo kunaashiria dalili za ufujaji wa fedha za wananchi ambao wengi walidai halmashauri imefanya hivyo ili kujenga mahusiano yaliyotoweka kati ya madiwani na mkurugenzi ambaye walimpigia kura ya kutokuwa na imani naye siku za hivi karibuni.
Walisema hawaoni sababu ya halmashauri kutumia fedha hizo kwa ajili ya safari ya madiwani kwenda Dodoma wakati Wilaya ya Kyela inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo ya ubovu wa miundombinu ya barabara, majisafi, mifereji ya kupitisha majitaka, kutokamilika kwa stendi kuu, na miradi ya maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu suala hulo, alisema aliombwa ruhusa ya safari ambayo imedhaminiwa na Dk. Mwakyembe.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Joseph Njau na mhasibu Jacob Mbarouk, walikiri ofisi hiyo kuwasafirisha madiwani hao kwenda Dodoma bila kutaja kiasi cha fedha kilichotumika.
Njau aliongeza kuwa ingawa safari hiyo ilidhaminiwa na Dk. Mwakyembe, si dhambi halmashauri kuwasafirisha madiwani kwa kuwa ndio wenye halmashauri.

0 comments: