MTOTO mkubwa wa Waziri Mkuu wa zamani
Hayati Edward Moringe Sokoine, Lazaro Sokoine, ameibuka na kutoa madai mazito
ya kutaka mwili wa baba yake ufanyiwe uchunguzi, kubaini chanzo cha kifo chake.
HAYATI MWALIMU JK NYERERE NA HAYATI EM SOKOINE
Mbali
na kutaka uchunguzi huo, Lazaro pia amemuandikia barua Rais Jakaya Kikwete
akielezea mlolongo wa matukio mengi, likiwemo mgogoro wa familia hiyo na
kuporwa kwa ardhi na mali zake zingine alizoachiwa na Hayati Sokoine.
Lazaro
alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalumu, huku
akishusha madai mazito dhidi ya Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Namelock Sokoine,
ambaye ni mdogo wake.
Kwa
nini mwili wa Sokoine uchunguzwe?
Akielezea
sababu za kutaka mwili wa Sokoine uchunguzwe, Lazaro alisema miezi minne kabla
ya kifo chake mwaka 1984 baba yake alienda nchini Cuba wakati Lazaro akiwa
masomoni nchini humo; Sokoine alimwambia mwanaye huyo kuwa asishangae kusikia
amekufa kwa njia yoyote ile ikiwamo kupigwa risasi kwani kuna watu wanamuwinda.
Alisema
baada ya baba yake kumueleza hivyo alihoji sababu ya kuwa na hofu hiyo ambapo
Sokoine alijibu kuwa hali ya nchi wakati huo chini ya Mwalimu Julius Nyerere,
ilikuwa mbaya kutokana na vita dhidi ya wahujumu uchumi.
Mtoto
huyo ambaye ana hali mbaya kiuchumi, alisema baba yake aliendelea
kumwambia kuwa kutokana na hali hiyo, Mwalimu Nyerere alimuongezea ulinzi
kutoka askari wanne hadi 14.
“Baba
alikuja Cuba kwa ajili ya sherehe za uhuru wa nchi hiyo na akaniambia maneno
hayo mazito nami nikaenda kuongea na walinzi wake ambao ni Mashaka, Kimaro na
Kalbert juu ya hofu hiyo ya baba,” alisema Lazaro.
Alisema
miezi minne baadaye alipata taarifa ya kifo cha baba yake kupitia Ikulu ya Cuba
hali iliyomfanya ayakumbuke maneno ya tahadhari aliyoambiwa juu ya hofu ya
kuuawa.
Akieleza
sababu nyingine iliyomfanya atake mwili wa baba yake uchunguzwe upya, Lazaro
alisema agizo la Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa wa wakati huo Imran Kombe,
kuwataka walinzi wa Sokoine waliokuwa Dodoma watangulie Arusha badala ya
kuandamana naye kwenda jijini Dar es Salaam, linatia shaka kwamba kulikuwa na
mpango wa kutaka kumuua.
Alisema
kutokana na mazingira hayo, amekuwa akitamani sana kuanzisha harakati za kutaka
mwili wa kiongozi huyo maarufu uchunguzwe, lakini hali yake kiuchumi ndiyo
inayomkwamisha.
“Kwa
sasa sina uwezo ila nikipata pesa nitaanzisha mchakato wa kuchunguza kifo cha
baba yangu; nimekuwa nikiuliza hili kwa muda mrefu, watu wamenichukia na sasa
wananipiga vita hadi ndani ya familia kwa kuhoji suala hilo, mdogo wangu
anayeitwa Joseph Sokoine aliyeko ubalozi wa Tanzania nchini Canada aliniambia
nisiulizeulize hili suala, wala nisiliingilie kwani siku moja wataning’oa macho
au kuniondoa duniani,” anaongeza Lazaro.
Alisema
hivi karibuni wakati mwili wa Sokoine ulipozikwa kwenye kaburi jipya kutoka
lile la awali, aliiambia familia yake kwamba isifunge milango ya kaburi ili
uchunguzi wa mwili wa baba ufanyike.
Hivi
karibuni gazeti la Tanzania Daima lilipata kuandika taarifa ya mwili wa Sokoine
kuzikwa kwenye kaburi jipya baada ya lile la awali kuharibika na kwamba familia
ina mpango wa kutaka kuufanyia uchunguzi mwili huo.
Ikumbukwe
kuwa wakati wa kifo chake kulikuwa na mjadala mzito, wengi wakidai aliuawa na
kwamba kifo chake kilipangwa na mahasimu wake ndani na nje ya serikali ambao
walikerwa na operesheni yake ya kupambana na wahujumu uchumi na mali za taifa.
Kwa
mujibu wa sheria, mwili ukishazikwa unaruhusiwa kufanyiwa uchunguzi baada ya
miaka 30 na mwakani mwili wa Sokoine utafikisha umri wa miaka 30 tangu
ulipozikwa na huo utakuwa muda muafaka kwa wana ndugu hao kutaka kujua ukweli
wa kifo cha ndugu yao.
0 comments:
Post a Comment