AFISA HABARI WA BUNGE WA ZAMANI AFARIKI DUNIA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
BUNGE LA TANZANIA
TANZIA
MAREHEMU NDG. ERNEST ZULU
(1957 – 2013)
Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashililah, anasikitika
kutangaza kifo cha mtumishi wa Bunge, ndg. Ernest Zulu, Afisa Habari Mkuu,
aliyefariki dunia tarehe 23/05/2013 akiwa masomoni nchini Malaysia, kwa maradhi
ya kichwa yaliyomsumbua kwa muda mrefu.
Mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu kuja Tanzania
kwa mazishi inaendelea. Taarifa ya ratiba kamili ya maziko itatolewa pindi
mipango hiyo itakapokamilika. Ndg. Ernest Zulu alizaliwa tarehe 10 Julai, 1957
Songea Ruvuma na alipata Elimu ya uandishi wa Habari katika chuo cha Uandishi
wa Habari cha TSJ (siku hizi SJMC) Jijini Dar es salaam na baadae kuajiriwa na
shirika la Utangazaji la Tanzania (RTD) mwaka 1976 kama mwandishi wa Habari
Msaidizi na hatimae kupandishwa cheo na kuwa Mwandishi wa Habari kabla ya
kuhamia shirika la magazeti ya Chama la Uhuru na Mzalendo kama Mwandishi Mwandamizi mwaka 1985, ambapo mwaka
1986 hadi 1987 alipata fursa ya kusomea masomo ya Uandishi wa Habari za
Kimataifa huko nchini Urusi.
Mwaka 1991 aliajiriwa kama Mhariri Msaidizi katika
gazeti la The Express kabla ya
kujiunga na Sauti ya Ujerumani ambako alifanya kazi kama Mwandishi Mwandamizi
kuanzia mwaka 1995.
Mwaka 1998 aliajiriwa na Ofisi ya Bunge kwa Cheo cha
Afisa Habari Mwandamizi ambapo mpaka mauti inamkuta alikuwa Afisa Habari Mkuu
daraja la pili.
Ndg. zulu alikwenda masomoni nchini Malaysia Julai,
2010 katika chuo kikuu cha Taylor akichukua Shahada ya kwanza ya Mawasiliano na
usimamizi wa vyombo vya habari ambapo alitarajiwa kumaliza masomo yake mwaka
huu Julai.
Marehemu ameacha Mjane na watoto Wanne.
Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu mahala pema
Peponi. Amina!
Imetolewa na
Idara ya Habari,
Elimu kwa Umma
na Uhusiano wa Kimataifa
Ofisi ya
Bunge
DODOMA
24 Mei, 2013
0 comments:
Post a Comment