Sunday, 19 May 2013

UGAIDI WATIKISA DODOMA



 Dodoma
TISHIO la ugaidi linaloikabili Tanzania limechukua sura mpya baada ya vyombo vya ulinzi kwa kushirikiana na maofisa usalama kulazimika kukesha wakifanya doria mjini hapa kuhakikisha ibada ya kusimikwa kwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana (KKKT), Dk. Jacob Chimeledya inafanyika salama.
Ulinzi huo uliendelea kutwa nzima jana kuzunguka Kanisa Kuu la Anglikana mjini hapa na maeneo jirani wakati wote wa ibada hiyo iliyohudhuriwa na Askofu Mkuu wa Cantebury nchini Uingereza,   Justin Welby huku Rais Jakaya Kikwete akiwa mgeni rasmi.
Tangu juzi usiku maofisa wa polisi waliovalia sare na kiraia pamoja na wale wa usalama walikuwa wakizunguka katika mitaa mbalimbali ya mjini, kuzunguka kanisa kuu hilo huku baadhi yao wakiwa na silaha za moto na mbwa.
Wakati wote ibada ikiendelea jana, barabara ya kutoka soko kuu la Majengo kupitia hospitali ya rufaa ya mkoa ilikuwa imefungwa huku ile ya kutoka Hoteli ya Dodoma hadi Nyerere ikiwa imefurika askari waliosheheni silaha.
Tofauti na ibada nyingine za siku zote, jana waumini waliohudhuria walilazimika kupekuliwa kwa umakini zaidi na maofisa usalama na kwa waumini waliokuwa na pochi na mikoba walitakiwa kufungua na kuonesha vitu vilivyomo licha ya kupitishwa katika mashine maalumu.
Tahadhari kwa vitisho hivyo vya kigaidi imenza kuchukuliwa kwa umakini zaidi na vyombo vya dola baada ya matukio ya mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea Zanzibar kwa viongozi wa dini kushambuliwa na lile la hivi karibuni la kulipuliwa kwa Kanisa Katoliki Parokia ya Olasiti jijini Arusha.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nalo limechukua tahadhari kwa kuwazuia wabunge kuegesha magari yao nje ya uzio wa Bunge na badala yake wawe wanayaegesha ndani au mkabala na jengo ng’ambo ya barabara ya Dodoma-Dar.
Akizungumzia vitendo hivyo vya ugaidi muda mfupi baada ya kusimikwa, Askofu Dk. Chimeledya alisema kuwa bado tatizo hilo linaonekana kuchukua nafasi kubwa, jambo ambalo linatishia amani ya Watanzania.
“Vitendo vya ugaidi vinaonekana kushamiri nchini na kulichafua taifa letu, na serikali lazima ioneshe juhudi za makusudi kuhakikisha watu ambao wanahusika na vitendo hivyo wanachukuliwa hatua.
“Hali hii ni mbaya na kwa siku za karibuni yametokea matukio mabaya sana kwa viongozi wa makanisa. Hii inasikitisha na inatia aibu kwa taifa letu ambalo limezoea amani, upendo na mshikamano,” alisema.
Alisema serikali inatakiwa kutambua kuwa hali ya kisiasa kwa sasa ni mbaya katika nchi pamoja na dunia kwa ujumla na watu wanaonekana kukata tamaa ya kuendelea kutawaliwa kutokana na kusongwa na umasikini ambao unaonekana kuwatesa.
Askofu Dk. Chimeledya alisema inasikitisha kuona kuwa nchi ina rasilimali nyingi lakini bado hazitumiwi na wazawa na badala yake kuna watu wachache kutoka mataifa mengine wanaokuja na kuzichukua kwa kujitajirisha huku wananchi wanaendelea kuwa masikini.
“Lazima serikali ichukue hatua kuhakikisha inakomesha mara moja vitendo vya baadhi ya watu wa kutoka nje kujichukulia rasilimali huku Watanzania wakiwa masikini,” alisema.
Akizungumzia malengo ya kanisa hilo, Dk. Chimeledya alisema limejipanga kujenga vyuo vikuu katika mikoa ya Kigoma na Mtwara pamoja na benki ambayo itakuwa na manufaa kwa Watanzania wote.
Askofu Mkuu wa Cantebury, Welby, alisema serikali inatakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na viongozi wa dini badala ya kuwagawa.
“Serikali ina kila sababu ya kuhakikisha inafanya kazi za kimaendeleo kwa ushirikiano mkubwa na viongozi wa dini. Ikumbukwe viongozi wa dini wana mchango mkubwa wa kimaendeleo kwa sekta zote kielimu, kiafya pamoja na kihuchumi,” alisema.
JK aonya
Rais Kikwete akizungumza katika ibada hiyo, alisema kuwa serikali itahakikisha inawasaka wote ambao walijihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani kwa kuhusika na ugaidi.
Alisema pamoja na kujitokeza kwa vitendo vya kihuni ambavyo vinafanywa na baadhi ya watu wachache kwa lengo la kutowesha amani, lakini serikali kwa kutumia vyombo vya ulinzi na usalama watahakikisha wanawasaka.
“Ni aibu kuona serikali ambayo waasisi wake walijenga misingi ya upendo, umoja na mshikamano lakini kutokana na watu kuwa na matakwa yao binafsi wanatumiwa ama wanajisikia kuvunja hali ya utulivu.
“Nataka kusema kuwa vitendo hivi vya kigaidi vinachochewa na kikundi cha watu wachache ambao kimsingi wao wanajua yakitokea machafuko kamwe hawawezi kukaa hapa nchini, watakimbilia nje,” alisema Kikwete.
Alitolea mfano wa wananchi wanaotoka mikoa inayopakana na mataifa jirani akisema kuwa vurugu zikitokea wao watakimbilia huko wakati wale wasio na uwezo huo wakitaabika.
“Wapo watu ambao yakitokea machafuko hapa nchini wao hawaoni tatizo, mfano James Mbatia yeye atakimbilia Kenya, Profesa Anna Tibaijuka yeye atakimbilia Uganda. Lakini wale ambao hawana pa kukimbilia mnafikiria watakimbilia wapi?” alihoji.
Aidha alizitaka dini zote kuhakikisha zinaiombea serikali na wale wote ambao wana roho ya uharibifu kuacha tabia hiyo na badala yake watunze amani iliyopo.
Pia alizigeukia dini alizodai zinaonekana kuwa na viashiria vya uchochezi na kusema kuwa dini hizo ni sawa na mashetani.
Rais Kikwete alisema kuwa anatambua mchango wa makanisa katika kuwasaidia Watanzania kihuchumi, kiafya na kielimu.

0 comments: