Friday, 24 May 2013

NIYONZIMA SASA 'AWARUSHA ROHO' YANGA SC

NIYONZIMA SASA 'AWARUSHA ROHO' YANGA SC, AREJEA RWANDA BILA KUSAINI MKATABA MPYA

Friday, May 24, 2013

clip_image001
Anaondoka? Haruna Niyonzima sasa anaiweka roho juu Yanga SC
Na Mahmoud Zubeiry,
KIUNGO wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Fadhili Niyonzima anaondoka kesho kurejea kwao, lakini bado hajasaini mkataba mpya na klabu yake, Yanga SC hali ambayo kwa kiasi fulani inazalisha hofu juu ya mustakabali wake katika klabu hiyo.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Dar es Salaam, Nahodha huyo wa Nyigu wa Rwanda, alisema kwamba bado yupo kwenye majadiliano juu ya mkataba mpya na bado hajasaini.
Niyonzima anayekwenda kujiunga na kambi ya timu yake ya taifa kwa ajili ya mechi za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil, alisema ana matumaini atafikia makubaliano mazuri na Yanga juu ya mkataba mpya na atabaki.
“Nadhani nitabaki, kama itakuwa tofauti, sijui,”alisema.
Niyonzima yupo katikati ya uvumi mzito kwamba anaweza kuhamia Simba SC ambao imeelezwa wako tayari kutoa dau la Sh. Milioni 70 na kumpa mshahara wa dola za Kimarekani 3,000 au Azam FC ambayo wazi itampa maslahi mazuri zaidi.
Juu ya uvumi huo, klabu yake, Yanga SC imesema imekwishasikia, lakini inafurahi ipo katika mawasiliano mazuri na kiungo wake huyo muadilifu.
“Nimesikia hata mimi hizo habari za kwenda Simba SC, lakini Haruna mwenyewe tupo naye vizuri na tunaendelea na mazungumzo ya mkataba mpya. Kwa kweli sisi hatuna wasiwasi na tutazungumza naye taratibu, hadi tufikie makubaliano, ambayo yatakuwa na maslahi mazuri kwa pande zote,”alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, Abdallah Ahmad Bin Kleb, alipozungumza na BIN ZUBEIRY jana.
Bin Kleb, alisema kwamba wachezaji wote muhimu ambao ama wamemaliza mikataba au wanakaribia kumaliza mikataba yao, wataongezewa mikataba mapema iwezekanavyo ili kuwajengea kujiamini.
“Unajua mchezaji kama mkataba wake umebaki muda mfupi, halafu klabu haijagusia kuhusu kumuongezea mkataba anaweza akawa na wasiwasi juu ya mustakabali wake na kwa mchecheto akasaini timu yoyote hata kama hapendi,”alisema.

0 comments: