Monday, 20 May 2013

MBARONI AKIDAIWA KUUZA MBOLEA FEKI MBEYA

Mbaroni akidaiwa kuuza mbolea feki



WIKI mbili baada ya gazeti la tanzania daima   kufichua uwepo wa dawa feki, mbegu na uchakachuaji wa mbolea kukithiri mkoani Mbeya, Jeshi la Polisi limefanikiwa kumnasa mmoja wa wanaodhaniwa kuwa ni wahusika wa mchezo huo mchafu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, alisema kuwa walimkamata Jofrey Mbago, mkazi wa Chimala wilayani Mbarali akiwa na mifuko 100 ya mbolea aina ya CAN ikiwa ndani ya mifuko yenye nembo ya Premium Agro Chem Ltd.
“Tulipata taarifa kutoka kwa Adjurist Edward Ngezi ambaye ni Ofisa Mauzo wa kampuni ya kusambaza mbolea iitwayo Premium Agro Chem Ltd yenye makao makuu jijini Dar es Salaam, akimlalamikia wakala wao Jofrey Mbago kuwa anasambaza mbolea isiyo halali kwa kutumia mifuko ya kampuni yao,’’ alisema.
Alisema uchunguzi wa awali uliofanywa na bwana shamba wa mji mdogo wa Chimala, Ezbon Michael, umebaini kuwa ndani ya mifuko hiyo kulikuwa na mbolea inayosadikiwa kuwa ni aina ya Minjingu.
“Mtuhumiwa alipohojiwa alikiri kuwa mbolea hiyo alipelekewa na Samwel Mhavile na Abson Sanga wakazi wa Makambako na kwamba mbolea hiyo inauzwa sh 50,000 kwa kila mfuko wa kilo 50 na hadi anakamatwa alikuwa ameshauza mifuko mingi,’’ alisema Kamanda Diwani.
Alisema kutokana na tukio hilo, taratibu zinafanywa sampuli ya mbolea hiyo ipelekwe kwa mkemia mkuu wa serikali jijini Dar es Salaam ili kuthibitisha mifuko hiyo ina mbolea aina gani.
Kukamatwa kwa mtu huyo kunatokana na habari ya kiuchunguzi iliyochapishwa na Tanzania Daima Mei 6, mwaka huu ikielezea namna wafanyabiashara wanavyojinufaisha kwa kufikia hatua ya kusaga matofali ya kuchoma kisha kuuza kwa wakulima wakidanganya ni dawa aina ya Rd Copper

source tanzania daima.

0 comments: