Thursday, 30 May 2013

YANGA SC YAMUONGEZA MKATABA NIZAR KHALFAN, YAMUITA MCHEZAJI WA KUIGWA NDANI YA TIMU


  

nizar
Nizar Khalfan katika picha tofauti, mbili kulia akiwa na Yanga SC na kushoto alipokuwa Marekani 
KLABU ya Yanga imesema kwamba, kiungo Nizar Khalfan ataongezewa Mkataba ili aendelee kuichezea klabu hiyo msimu ujao baada ya msimu huu kuuridhisha uongozi na benchi la Ufundi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, Abdallah Ahmad Bin Kleb amenena jana kwamba, Nizar anawavutia hata viongozi kutokana na nidhamu yake ya hali ya juu.
“Yule mchezaji kwa kweli ni mfano wa kuigwa katika suala la nidhamu. Na pia huwa anaonyesha uwezo mkubwa sana anapopewa nafasi. Naweza kusema, katika wachezaji ambao wamemaliza Mikataba, yule ni miongoni mwa waonabaki,”alisema.  
Kuhusu wachezaji wengine waliomaliza mikataba akina Nurdin Bakari, Oscar Joshua, Stefano Mwasyika, Godfrey Taita na kipa Said Mohamed, Bin Kleb alisema hatima yao itajulikana wiki mbili zijazo.
Kuna ripoti mwalimu kaiandika kuhusu timu kwa ujumla, ndani yake kuna wachezaji ambao amesema hatawahitaji tena. Tutaipitia na kwa wale ambao mwalimu amesema atawahitaji tutaagana nao kiungwana na kuwapa asante yao kwa kuitumikia klabu,”alisema.
Bin Kleb alisema wapo wachezaji wengine ambao hata kama hawataguswa na ripoti kocha, lakini uongozi umegundua ni mushkeli katika klabu, nao pia watapewa ‘mkono wa kwaheri’.
Kuhusu usajili, Bin Kleb alisema bado wanaendelea kwa umakini wa hali ya juu na wanafanya hivyo kulingana na mapendekezo ya kocha wao, Ernie Brandts ambaye kwa sasa yupo mapumzikoni kwao, Uholanzi.
“Usajili unaendelea na kama unavyojua, haya si mambo ya kukurupuka, basi tunafanya taratibu na lengo letu ni kuhakikisha siyo tu tunaendelea kutawala katika soka ya Tanzania na Afrika Mashariki na Kati, bali pia kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika,”alisema Bin Kleb. 
Yanga ilimsajili Nizar kutoka Marekani msimu huu ambako alikuwa akicheza soka ya kulipwa na katika msimu wake wa kwanza, anajivunia kutwaa mataji mawili, Kombe la Kagame na Ligi Kuu.
Yanga inatarajiwa kuanza mazoezi Juni 3,  mwaka huu kujiandaa na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, michuano ambayo itafanyika nchini Sudan mwezi ujao.
Katika michuano hiyo, mabingwa hao mara mbili mfululizo wa Kagame, wamepangwa Kundi C pamoja na Ports ya Djibouti, Express ya Uganda na Vital 'O' ya Burundi, wakati wapinzani wao wa jadi, Simba SC wamepangwa Kundi A pamoja na wenyeji El-Mereikh, Elman  ya Somalia na APR ya Rwanda
Katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Juni 18 hadi Julai 2, mwaka huu mjini Khartoum, Sudan, mabingwa wa Kenya, Tusker wamepangwa Kundi B pamoja na wenyeji wengine, Al-Hilal, Falcons ya Zanzibar, Al Ahly Shandy ya Sudan na Al-Nasir Juba ya Sudan Kusini.
Mabingwa watetezi, Yanga wataanza kampeni zao za kutetea taji hilo Juni 20 kwa kumenyana na Express, wakati Simba SC itashuka dimbani Juni 21 kufungua dimba na El-Mereikh, na mechi zote zitachezwa Elfashar.

0 comments: