Sunday, 26 May 2013

MLUGO APIGA MARUFUKU WANAFUNZI WANAO TUMIA SIMU MASHULENI

NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, amesema atafanya ziara katika shule zote za msingi na sekondari ili kuwabaini wanafunzi wanaotumia simu za mkononi shuleni.

Mulugo alitoa kauli hiyo mjini hapa juzi alipokuwa akizindua mpango mkakati wa elimu ya haki za binadamu na kuongeza ataanzia Mkoa wa Dodoma na atakaowabaini atawanyang’anya na kuzichoma moto.

Alisema suala la utandawazi limechangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi kuharibika na kuwa na nidhamu mbovu, ikiwa ni pamoja na kuwadharau walimu na wazazi.

Mulugo alisema kitendo cha wanafunzi kwenda na simu shuleni kimesababisha mmomonyoko mkubwa wa maadili, ambapo pia kimechangiwa na baadhi ya wazazi kujifanya wanawapenda watoto wao: “Hivi sasa limekuwa ni jambo la kawaida kuwakuta wanafunzi wa ngazi zote wakiwa na simu shuleni. Mimi sikubaliani nalo, nimeamua nitafanya 

ziara shule moja baada ya nyingine nikimkagua mwanafunzi mmoja baada ya mwingine nikianzia na Mkoa wa Dodoma katika kipindi hiki cha Bunge. Ole wake mwanafunzi nitakayemkuta na simu nitamnyang’anya na kuichoma moto maana walimu wanawalea sana… halafu na mimi mniimbie ‘tunataka haki zetu’,” alisema Mulugo.

Naibu Waziri huyo alisema suala la wanafunzi kuwa na simu limesababisha kujiingiza katika vishawishi na kuanza vitendo vya ngono wakiwa na umri mdogo.

Aidha, alisema mpango huo uliozinduliwa unawawezesha wanafunzi kujua wajibu na kudai haki zao.

Mulugo aliwaasa wanafunzi wote wakiwemo wa vyuo vya elimu ya juu kuacha kudai haki ikiwemo mikopo kwa kufanya vurugu na maandamano na badala yake watumie vyombo vya sheria pale wanapoona haki imepindishwa.

---
Imeandikwa na Happiness Mtweve
 
Source TanzaniaDaima

0 comments: