PROFESA LIPUMBA AIBUA JIPYA NA ZITO
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF),
Profesa Ibrahim Lipumba, ameibua suala zito akikihusisha chama chake na
“kumnusuru” Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu uliopita.
Tanzania
Daima limefahamishwa kuwa Profesa Lipumba alitoboa siri hiyo katika Msikiti wa
Idrissa, Kariakoo, jijini Dar es Salaam, alikokwenda kuswali swala ya Ijumaa,
miezi kadhaa iliyopita.
Kwa
mujibu wa video ya tukio hilo, ambayo gazeti hili lina nakala yake, Profesa
Lipumba alikaribishwa kuzungumza na waumini hao mara baada ya utangulizi
uliotolewa na Imamu wa msikiti huo, Sheikh Ali Basaleh, aliyemtaka awaeleze
Waislamu hali ya kisiasa nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Huku
akisisitiza juu ya umuhimu wa mshikamano wa kiimani, Profesa Lipumba alianza
kwa kuzungumzia matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2010, na ushindani mkali wa kisiasa
uliokuwapo.
Alisema
hawaoni matunda ya jitihada walizofanya kumnusuru Rais Kikwete asishindwe,
kwani hata chini ya uongozi wake, Waislamu wameendelea kutothaminiwa.
“Ninyi
masheikh mnajua vizuri zaidi hali ya kisiasa ilivyokuwa, kwamba ilibidi
zifanyike juhudi za makusudi ili kuokoa jahazi. Lakini pamoja na kuliokoa
jahazi, hali halisi inaonyesha mpaka sasa hakuna matunda yoyote yaliyopatikana,
na tupo katika mtihani mgumu zaidi,” alisema.
Katika
hali ambayo inasemekana ushindi wa Rais Kikwete ulipatikana kwa mbinu, huku
wengine wakiituhumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa ilimnusuru mgombea wa CCM,
kauli hii ya Profesa Lipumba inadokeza kwamba anajua mkakati zaidi wa kazi ya
Tume ya Uchaguzi.
Katika
hali isiyo ya kawaida, Profesa Lipumba anaonekana kuhamasisha Waislamu
kujipanga akisema “wenzetu wameanza kujipanga” kuelekea 2015.
CHANZO: TANZANIA DAIMA JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment