RAIS Jakaya Kikwete ameomba msaada wa
walimu wa Hisabati na Sayansi kutoka nchini Jamaica ili kukabiliana na upungufu
wa wataalam hao nchini.
Rais
Kikwete alitoa ombi hilo Jumatatu ya juma hili kwenye Hotel ya Sheraton mjini
Addis Ababa, Ethiopia wakati wa mkutano wake na Waziri Mkuu wa Jamaica, Mama
Portia Simpson Miller.
Ikulu
ilisema kuwa Rais Kikwete alikuwa Addis Ababa kuhudhuria sherehe za miaka 50
tokea kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika, Juni 25, 1963 na Mkutano wa 21 wa Wakuu
wa Nchi Wanachama wa AU wakati Mama Simpson Miller alipokuwa mmoja wa viongozi
mashuhuri wa nchi mbali mbali duniani walioalikwa kuhudhuria sherehe hizo.
Taarifa
ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu iliyosambazwa jana kwa vyombo vya habari,
ilisema kuwa katika mazungumzo ya viongozi hao wawili, Mama Portia Simpson
Miller ambaye aliapishwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamaica Januari 5, 2012 baada ya
chama chake cha Peoples National Party (PNP) kushinda uchaguzi mkuu nchini
humo, alimwuliza Rais Kikwete jinsi gani Jamaica inavyoweza kuisaidia Tanzania.
Kutokana
na swali hilo, Rais Kikwete aliomba mambo mawili, mosi kupatiwa walimu wa
masomo ya hisabati na sayansi pamoja na kocha wa riadha.
Kutokana
na ombi hilo, mama huyo alimwahidi Rais Kikwete kuwa Jamaica ina uwezo wa
kusaidia katika maeneo yote mawili.
Kutokana
na makubaliano hayo, serikali sasa inatarajiwa kupata walimu wa masomo hayo
mawili na kocha wa mchezo wa riadhaa. Hata hivyo taarifa hiyo haikutaja idadi
ya walimu wa masomo hayo.
Katika
matokeo ya kidato cha nne na sita, kumekuwa na idadi kubwa ya wanafunzi
wanaofeli masomo hayo kwa madai kuwa walimu wanaoweza kufundisha masomo hayo ni
wachache.
Lakini
kibaya zaidi wataalam wa masomo hayo licha ya uchache wao, hawana motisha na
ndio sababu yao kutofundisha vizuri na kusababisha matokeo mabaya katika masomo
hayo.
Mbali
ya makubaliano hayo, nchi hizo mbili zimeahidi kuongeza ushirikiano katika
nyanja mbalimbali na kuangalia uwezekano wa Tanzania kufungua aina ya
uwakilishi katika Kisiwa hicho cha Caribbean katika miaka miwili ijayo.
Kuhusu
kocha wa riadha, Mama Simpson Miller amesema kuwa na hilo halina pingamizi kwa
sababu yeye alikuwa Waziri wa Michezo kwa miaka mingi na kuwa kwa sasa Wizara
ya Michezo iko kwenye Ofisi yake ya Waziri Mkuu.
Jamaica
ni moja ya nchi zinazoongoza katika mchezo wa riadha duniani ikiwa imetoa
wanariadha wengi mabingwa wa dunia akiwamo bingwa wa sasa wa Olimpiki na dunia
katika mbio fupi za mita 100 na 200, Usain Bolt.
kwa msaada wa Jaizmilaleoblog
0 comments:
Post a Comment