TFF NA PANGA LA WAROPOKAJI
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF),
limesema Kamati ya Maadili ya shirikisho hilo iliyo katika mchakato wa kuundwa
kwa agizo la Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), itakuwa tiba sahihi kwa
viongozi waropokaji na wasio waadilifu.
Akizungumza
na waandishi wa habari makao makuu ya TFF jijini Dar es Salaam jana, Katibu
Mkuu wa shirikisho hilo, Angetile Osiah, alisema zama za waropokaji miongoni
mwa viongozi wa soka la Tanzania zinakaribia kwisha na kwamba cha moto kinakuja.
Alisema
kuwa viongozi wa klabu nchini, hasa za Ligi Kuu, wamekuwa na kasumba ya kukwepa
majukumu yao na kulitupia mzigo shirikisho, ambalo linapofuata sheria na
kanuni, huonekana kama linafanya kazi kwa ukandamizaji.
Osiah
alitoa kauli hiyo wakati akilitolea ufafanuzi sakata la usajili tata wa Mrisho
Ngasa, aliyetua Yanga akitokea Simba, ambayo inadai ina mkataba naye wa mwaka
mmoja anaopaswa kuutumikia baada ya kumaliza ule wa mkopo akitokea Azam FC.
“Kanuni
za usajili zipo na wote mnazo na mnazitambua. Katika hili la Ngasa mnapaswa
kurejea kuzisoma ili kujua zinasemaje, sio baadhi ya viongozi kuwaelekeza kwetu
wakati kimsingi ni kama hatuhusiki katika mfumo wa sasa wa usajili,” alisema.
Aliongeza
kuwa TFF inaamini viongozi wa klabu waliomba kazi hizo na kuchaguliwa, kwa
kuaminiwa watawajibika na hawapaswi kukwepa majukumu yaliyowaweka madarakani
kwa kuyakimbizia katika shirikisho.
Aidha,
aliziasa klabu nchini, kujenga utamaduni wa kuwaacha makocha kufanya usajili wa
wachezaji, ili kuwawezesha kuimarisha vikosi kutokana na upungufu waliouona
kikosini, sio viongozi wanaosajili kwa faida binafsi.
0 comments:
Post a Comment