Sunday, 12 May 2013

Silaa ajipanga kumng’oa Mahanga






MEYA wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa, anadaiwa kuandaa mkakati wa kumuangusha mbunge wa Segerea, Makongoro Mahanga  katika kuwania ubunge wa jimbo hilo kwenye  uchaguzi mkuu wa 2015.

Mkakati unaodaiwa kufanywa na meya huyo anayedaiwa kuliwania jimbo hilo ni pamoja na kukutana na wanachama wa CCM katika vikao vya ndani  vya jimbo la Segerea na kuukosoa utendaji wa Mahanga kuwa unaliweka jimbo rehani.

Chanzo chetu kilibainisha kuwa katika  baadhi ya mikutano  ya ndani ya chama hicho Silaa amedhamiria kulitwaa jimbo hilo na ameanza kuwashawishi wapiga kura ndani ya chama waone hatari ya kumrejesha Mahanga mwaka 2015.

“Inasemekana ushindani uliokuwepo mwaka 2010 ulitishia uhai wa CCM Segerea hasa wakihusisha na ukosefu wa muda wa Mahanga kuwatumikia wananchi kutokana na majukumu ya uwaziri aliyonayo,” kilisema chanzo hicho.

Mwenyekiti wa CCM tawi la Liwiti, Kitwana Manara amethibitisha kuwapo kwa mkutano wa ndani wa chama hicho uliohudhuriwa na Meya Silaa, huku akikanusha kuwepo kwa mkakati wa kumpinga Mahanga.

Manara alisema Meya Silaa alifika katika mtaa wa Liwiti Desemba mwaka jana na kufanya mkutano wa ndani ambapo viongozi wa chama walimueleza matatizo ya soko linalowakabili wananchi wa Liwiti.

Alisema baada ya mkutano huo Meya Silaa aliitisha mkutano wa hadhara na wananchi na kisha kuwaeleza namna ya kutatua kero hiyo.

Akizungumzia , kuhusu mikutano ya Silaa, Mahanga alisema taarifa za watu kufanya vikao vya kuwania jimbo hilo amezisikia na kuwataka wawe wazi juu ya dhamira zao.

Alisema si Silaa pekee wanaofanya mikutano hiyo bali kuna baadhi ya wana CCM wanaofanya vikao hivyo vya chini chini kwa ajili ya kuwania jimbo hilo na kusema kila mmoja ana haki ya kugombea.

“Wewe umeniambia ni Jerry, mimi sijapata taarifa zake ila wapo wengi zaidi ya jina hilo na wanafanya mkakati huo, lakini jambo la msingi kwa sasa mimi ndiye mbunge wa Segerea na wanaotaka kugombea wakati ukifika wana haki ya kufanya hivyo ila wawe wawazi juu ya dhamira zao,” alisema.

Silaa alipoulizwa  kwa njia ya simu juu ya mkakati huo anaodaiwa kuuendesha, alitaka atumiwe maswali kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno ili aweze kujibu kwa ufasaha.

“Nitumie meseji nikujibu ili uweze kuandika habari yako vizuri, kwa sasa hatutaweza kuongea kwa kuwa nipo sehemu yenye makelele,” alisema Silaa.

Kufuatia kuomba kutumiwa ujumbe huo alitumiwa ujumbe mfupi wa simu muda wa saa 2:43 ambao ulipokelewa katika simu ya meya huyo ambaye hakuweza kuujibu na hata alipopigiwa simu kwa ajili ya kukumbushwa simu yake iliita bila kupokelewa.

0 comments: