Sunday, 12 May 2013

Dr. Slaa amlipua JK • ASEMA AMEMWAGA SUMU YA UDINI MISIKITINI









KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa amesema Rais Jakaya Kikwete ndiye analiyeliangamiza taifa.

Alibainisha kuwa kitendo cha Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoongozwa na Kikwete kushindwa kuchukua uamuzi makini katika masuala muhimu kwa taifa ndiko kunakoliangamiza na kuliteketeza.

Dk. Slaa alitoa kauli hiyo katika mikutano yake miwili aliyoifanya katika wilaya za Momba na Mbozi zilizopo mkoani Mbeya.

Alisema mgogoro wa uchinjaji wa nyama baina ya Waislamu na Wakristo iliyotokea hivi karibuni ni miongoni mwa masuala yanayoliweka taifa kubaya, lakini imechangiwa na serikali dhaifu ya CCM.

Aliongeza kuwa Rais Kikwete amekuwa na tabia ya kuchelewa kuchukua uamuzi sahihi na kwa wakati yanapojitokeza matatizo yanayotishia umoja, amani na mshikamano uliopo kwa muda mrefu hapa nchini.

Alibainisha kuwa migogoro mingi inayotokea hapa nchini inajengwa au kutengenezwa na serikali iliyojikita kusambaza sumu ya udini katika misikiti wakati wa kampeni za urais mwaka 2010.

Aliongeza kuwa katika kampeni hizo, Rais Kikwete na timu yake ilikuwa ikisaka kura kwenye nyumba za ibada na kumwaga sumu mbaya ya udini ambayo sasa inaitesa serikali na taifa.

“Hawa walitafuta kura kwa njia haramu, walimwaga sumu ya udini misikitini. Leo hii taifa linaanza kuhangaika kutatua mizozo ya Wakristo na Waislamu iliyozalishwa na utawala wa Rais Kikwete.

“Ubinafsi wa watu wachache unalisababisha taifa liingie katika hofu ya kutoweka kwa amani, Rais Kikwete hawezi kukwepa lawama za kutufikisha hapa tulipo,” alisema.

Aidha, Dk. Slaa alisema Tanzania inatajwa kuwa nchi masikini wakati si kweli kutokana na rasilimali ilizonazo ambazo zinawanufaisha watu wachache hasa wale waliopo madarakani.

“Tazameni ni mabilioni mangapi yanapotea Tunduma mpakani kwa ucheleweshwaji wa kuyahurusu magari ya mizigo kupita ili yaweze kufanya mzunguko huo mara nyingi, wangekuwa makini hakika Tunduma pangekuwa pamebadilika,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa kazi ya CHADEMA ni kukosoa na kuibua hoja mpya kwa ajili ya ustawi wa maendeleo ya wananchi, hivyo wataendelea kufanya hivyo hadi pale serikali iliyoko madarakani itakapoamua kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili Watanzania.

“Kama kweli CCM itaweza kuteremsha bei ya simenti hadi kufikia chini ya shilingi 5,000 na bati zikauzwa kwa bei hiyo, elimu na afya vikatolewa bure kwa wananchi wetu, vijana wakapata ajira kutokana na kufufua viwanda vyetu vilivyokufa, basi CHADEMA hatutakuwa na sababu ya kugombana nao majukwaani,” alisema.

Kiongozi huyo aliwataka viongozi wa dini zote nchini kusimamia kikamilifu jukumu kubwa walilopewa na Mungu la kukemea haraka uvunjwaji wa haki ambayo ndiyo huzaa amani.

Awali akifungua matawi ya CHADEMA yapatayo 12 na kuzindua ofisi za chama hicho Wilaya ya Momba, Dk. Slaa aliwataka wananchi kuzitumia vema ofisi hizo kwa kupeleka malalamiko yao ili yapatiwe ufumbuzi mapema.

Naye Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde alisema CHADEMA kwa sasa hawana muda wa kuwajibu CCM hoja kwenye majukwaa bali sasa ni vitendo.

Silinde aliwataka wananchi wasiache kuwaonya wabunge wa CHADEMA kama kile wanachowatuma bungeni hawakifikishi.

Dk. Slaa alifika Tunduma juzi akitokea nchini Zambia alikokwenda kwa ziara ya siku tatu kutokana na mwaliko rasmi wa rais wa nchi hiyo, Michael Satta.

0 comments: