WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, jana alishindwa kuinasua Idara ya Usalama wa Taifa (TISS)kwenye tuhuma mbalimbali zinazowakabili baadhi ya maafisa wake waandamizi.
Kwa siku za hivi karibuni, idara hiyo imekuwa ikituhumiwa na baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wakidai kuwa baadhi ya watendaji wake waandamizi wanajihusisha na mikakati miovu.
Katika mwendelezo wa tuhumza hizo, Waziri Mkuchika alishindwa kutoa ufafanuzi wa kueleweka wakati akijibu swali la msingi la mbunge wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere (CHADEMA), bungeni mjini hapa.
Nyerere alitaka kujua idara hiyo imetoa msaada gani kwa taifa kuhakikisha kuwa rasilimali za taifa hazimilikiwa kifisadi na wachache ili taifa liwe salama kwa vizazi vijavyo.
Katika majibu yake, Waziri Mkuchika alisema kuwa majukumu ya idara hiyo yameainishwa katika kifungu cha 5 cha sheria Na.15 ya mwaka 1996 ya kuundwa kwa idara hiyo.
“Majukumu hayo ni kukusanya taarifa za kiusalama, kuzifanyia uchunguzi na kuishauri serikali kwa lengo la kuchukua hatua zinazostahili. Miongoni mwa taarifa hizo ni pamoja na zinazohusu vitendo vya hujuma dhidi ya uchumi na rasilimali za taifa kama vile kumilikiwa na watu wachache kwa manufaa yao binafsi,” alisema.
Mkuchika aliongeza kuwa hatua hiyo huchukuliwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa rasilimali zilizopo zinanufaisha taifa sasa na baadaye.
“Hivyo basi idara hiyo imekuwa ikitekeleza majukumu hayo kwa weledi na umakini mkubwa ili kuhakikisha taifa linaendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu,” alisema.
Baada ya majibu hayo, Nyerere aliuliza swali la nyongeza akisema: “Kwa kuwa waziri amekiri kuwa Idara ya Usalama wa Taifa imekuwa ikifanya kazi zake kwa umakini na weledi mkubwa na kwa taarifa nilizonazo idara hiyo iko kwenye uwanja wa ndege wa KIA na ilitoa ushauri kwa serikali kuhusu uwepo wa ndenge ya Qatar iliyochukua wanyama wetu na kwa kuwa serikali ilishauriwa kabla lakini ikapuuza ni hatua gani zilichukuliwa kwa watumishi wa serikali walioshindwa kuchukua hatu?”
Nyerere pia alitaka kujua kama hatua hazijachukuliwa kwa wahusika, serikali inawashauri nini wananchi wachukue hatua gani dhidi yake.
Hata hivyo, Mkuchika hakutoa majibu ya moja kwa moja kuonyesha hatua zilizochukuliwa na badala yake alirudia kueleza majukumu ya idara hiyo.
“Katika majibu yangu ya msingi nilizieleza kazi za Idara ya Usalama wa Taifa na si vibaya kwa manufaa ya Watanzania nikazirudia.
“Sheria iliyounda idara hiyo inafafanua majukumu ya chombo hicho kuwa ni kukusanya taarifa na kumjulisha waziri, kumshauri waziri kuhusu masuala ya usalama, kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi kadiri inavyowezekana ndani na nje ya nchi na mwisho ni kumshauri Rais au waziri anayehusika endapo kuna vitendo vinavyohusu ujasusi, uhujumu uchumi na ugaidi,” alisema.
Alisema kuwa Idara ya Usalama wa Taifa haimkamati wala kumshtaki mtu bali inafanya kazi ya kukusanya taarifa na kushauri na iwapo ikishauri halafu mtu hajachukua hatua, mamlaka iliyo juu yake ndiyo inapaswa kumchukulia hatua.
Kuhusu wananchi wachukue hatua gani dhidi ya serikali, Mkuchika alisema wajibu wa kila mwananchi ni kushirikiana na serikali kulinda taifa lake.
0 comments:
Post a Comment