UONGOZI wa Yanga sc umesema haumbanii winga wao
hatari, Mrisho Khalfan Ngassa `Anko` kujiunga na klabu ya Free State Stars
inayoshiriki ligi kuu nchini Afrika kusini.
Siku za karibuni kumekuwepo na taarifa za Ngassa
kufanya majaribio na kufuzu katika klabu hiyo inayonolewa na kocha wa zamani wa
Yanga, Mbelgiji, Tom Saintfiet na kukubali kulipa dola elfu 80 ambazo ni sawa
na milioni 130 za Kitanzania.
Lakini taarifa zinaeleza kuwa Yanga wamegoma kiasi
hicho cha fedha na kusema wanahitaji dola laki moja na nusu sawa na milioni 240
za Kitanzani na ndipo Free State wametia
ngumu juu ya kiasi hicho cha fedha.
Lakini inasemekana Free State ipo tayari kuongeza
dau kidogo ili kupata huduma ya winga huyo mwenye kasi uwanjani.
Katibu mkuu wa Yanga, Beno Njovu amesema hadhani
kama uongozi unambania Ngassa kwani wakifuatilia kwa undani zaidi wanagundua
kwamba kama unamtaka mchezaji duniani, sehemu yoyote, inageuka kuwa biashara,
haigeuki kuwa ofa, haigeuki kuwa kubaniana ila ni biashara.
“Kama klabu ipo `serious` kumtaka, sioni kama kuna
suala la kubaniana. Sidhani kama dau tunalosema ni kubwa kwa mchezaji kama
Ngassa. Ni dau dogo sana kwa gharama ambazo tayari tumeshaingia kwake”. Alisema
Njovu.
“Huwezi kufanya mambo bila kufuata taratibu za
makubaliano.Tunafanya hivyo kwasababu sisi tunaelewa gharama ambazo tumeingia
juu yake, tunaelewa kama kuna madeni yaliyopo yanayomhusu Ngassa, tunayajua,
kwahiyo kuna vitu vingi sana vinatakiwa kuhusishwa kwenye hiyo hesabu, mtu wan
je hawezi kujua”. Aliongeza Njovu.
Njovu alikanusha kusema wao wanataka kumuuza Ngassa
kwasababu yeye ni binadamu, lakini wanajaribu kuzungumzia thamani yake.
Pia
alisema wataongea na Ngassa akisharudi
nyumbani akiwa katika majukumu ya kuitumikia timu ya Taifa, lakini
tayari nyota huyo yupo nchini na jana alifika katika uwanja wa mazoezi
wa
Bandari Tandika akiwa amevalia nguo za nyumbani.
Mtakatifu, Tom Saintfiet anaiwinda saini ya Ngassa ili ajiunge na klabu yake ya Free State Stars ya Afrika kusini.
“Sisi tunajua Ngassa yupo na timu ya Taifa, na
kwasababu yupo na timu ya taifa, tunasubiri timu ya taifa irudi ili tuongee
naye kama mchezaji, halafu tujue anaipimaje hiyo timu”. Alisema Njovu.
Aidha Njovu aliongeza kuwa wameikataza Free state
kuongea na vyombo vya habari kwasababu haya ni mazungumzo ambayo yapo ndani ya
klabu na sio vizuri kuongelea kwenye vyombo vya habari.
“Kama wao tumewakataza, basi nasisi hatupaswi
kuongea hizo habari kwenye vyombo vya habari na hatutaki kutumia vyombo vya
habari kufanya mazungumzo”.
“Tukimaliza mazunguzo ya ndani, hapo tunaweza
kuzungumza kwenye vyombo vya habari”.
“ Hutajaweka kitu chochote kuwa kificho kwasababu
hakuna kitu chochote kilichopo mezani, mpaka tupate vitu kamili na kuongea na
watu ambao tunajua ni watu wanaohusika”.
“Bado hatujakaa mezani kuweza kuzungumza. Kwanza tunatakiwa kuongea na mchezaji, ngoja arudi kwanza kutoka timu ya Taifa baada ya kumaliza kazi hiyo tutamuulize”. Alihitimisha Njovu.
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0 comments:
Post a Comment